
Na Mwandishi wetu- KILIMANJARO
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ametoa wito kwa jamii kuwapenda, kuwajali na kuwahudumia makundi ya wenye mahitaji maalumu ili kukuza umoja na mshikamano katika Jamii.
Mhe. Nderiananga alisema hayo leo Disemba 31, 2025 akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa utaratibu wa utoaji zawadi za sikukuu mbalimbali kuelekea Sikukuu ya Mwaka Mpya wa 2026, zawadi hizo zimeenda kwa watoto 190 wakiwemo wenye ulemavu na wasio na ulemavu wanaolelewa na Shirika la The Creator Share Foundation lililopo Kata ya Kirua, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.
Alisema, ndani ya siku 100 za uongozi wake ameendelea kuleta faraja, upendo, tumaini na umoja kwa watanzania huku akisema kuwa kitendo hicho ni ishara ya upendo mkubwa kwa wananchi bila kujali hali zao.

“Naomba nitumie fursa hii kuwatakia kheri ya sikukuu ya mwaka mpya wa 2026 twende tukasherehekee kwa amani na tukiwa na faraja kwa sababu Mhe. Rais ametukumbuka sisi ni watoto wake hivyo tudumishe upendo huu miongoni mwetu kila mmoja amuone mwenzake ni wa muhimu katika jamii,” alisema Mhe. Nderiananga.

Akitaja vitu alivyovikabidhi kwa watoto hao alisema, ni pamoja na Mchele kilo 100, Ngano kilo 50, Mbuzi wawili, sabuni, mafuta ya kupikia, madaftari, sukari kilo 25 na vinywaji

" Nitoe wito kwa jamii kuwa, kila mmoja ana wajibu wa kuwahudumia watoto na watu wenye mahitaji maalum, siyo tu kwa siku za sikukuu, bali kwa muda wote ili kuwapa faraja na huo ndio upendo tunaotakiwa kuwaonesha," aliongeza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Bw. Godfrey Mnzava alibainisha kuwa, ili kuwa na ustawi wa maisha ya kijamii ni lazima kuwajali watu wenye uhitaji ili waweze kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku.

Naye,Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Vunjo Magharaibi ambaye pia ana mtoto mwenye ulemavu anayelelewa katika Shirika hilo Bi. Pamela Chuwa alipongea hatua hiyo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwafikia watu wenye ulemavu hatua inayowaganya kujisikia kuwa ni sehemu ya jamii.

“Mimi kama mama mwenye mtoto wa mahitaji maalum nimejisikia furaha kwa kupewa kipaumbele na tumefurahi sana Naibu Waziri Ummy kutufikia ukizingatia baadhi yetu tumefukuzwa katika familia tukionekana kama kuzaa watoto wenye ulemavu ni mkosi na laana katika familia,” alipongeza Bi. Diwani huyo.

Vilevile Afisa Rasilimali Watu katika Shirika hilo Bi. Judith Shio mara baada ya kupokea zawadi hizo alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa upendo na kuwajali watu wenye mahitaji Maalum huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitolea ili kuendelezwa moyo wa upendo na faraja kwa makundi hayo.
“Kwa niaba ya Shirika tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa upendo huu na mwaka huu tunauanza kipekee sana na watoto wamefurahi hivyo kwetu imekuwa faraja kubwa na imegusa jamii,” alishukuru Bi. Judith.
Nao baadhi ya watoto wanaolelewa katika Shirika hilo wameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka wakisema ujio huo kwao umekuwa ni historia na furaha kubwa ya kuuanza mwaka mpya kwa matumaini huku wakimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo huo wa the kuwashika mkono watoto wenye mahitaji maalum.
MWISHO
0 Comments