Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YATINGA KUNDI LA JUU LA UKOMAVU WA TΕHΑΜΑ pUΝΙΑΝΙ ΚWA MARA YA PILI.




Na Mwandishi Wetu 


Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa baada ya Benki ya Dunia (World Bank - WB) kuitaja kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ukomavu wa juu wa matumizi ya TEHAMA katika sekta ya umma, hatua inayothibitisha mafanikio ya mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kutekelezwa na Serikali.


Kwa mujibu wa Ripoti ya Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika Utoaji wa Huduma za Serikali na Ushirikishwaji wa Wananchi ‘GovTech Maturity Index - GTMI’ ya Benki ya Dunia mwaka 2025, Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A - Ukomavu wa Juu wa matumizi ya TEHAMA (Extensive GovTech Maturity), kundi linalojumuisha nchi zinazoongoza duniani katika matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi.

Ripoti hiyo hutathmini kiwango cha ukomavu wa TEHAMA serikalini takriban katika nchi zote duniani, kwa kuzingatia maeneo mbalimbali yakiwemo sera, sheria, miongozo, mifumo, na utekelezaji wake ambapo, katika mwaka uliopita ripoti hiyo ilitolewa mwezi Desemba, 2025.


Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kutambuliwa na Benki ya Dunia (WB) katika kupiga hatua ya ukomavu wa TEHAMA, ambapo mwaka 2022 Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri zaidi duniani katika GovTech Maturity Index. Katika utafiti huo uliohusisha nchi 198, Tanzania ilipanda kutoka nafasi ya 90 mwaka 2021 hadi nafasi ya 26 mwaka 2022 na kutoka kundi B hadi kundi A. Barani Afrika, Tanzania ilishika nafasi ya pili baada ya Mauritius na kuwa kinara wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Kuimarika kwa Nafasi ya Tanzania Kimataifa
Mafanikio haya ni mwendelezo wa safari ya Tanzania ya kupanda ngazi katika ukomavu wa TEHAMA serikalini, na kuendelea kujijengea taswira chanya kimataifa na kikanda.

Tanzania imeendelea kuonesha uthabiti katika matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuboresha ufanisi wa taasisi za umma, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wa bara la Afrika, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi vinara wa mageuzi ya kidijitali serikalini, ikilinganishwa na mataifa mengine yaliyofanyiwa tathmini katika ripoti hiyo. Tanzania ni moja kati ya nchi tano tu katika bara la Afrika ambazo zimeingia kwenye kundi la juu la ukomavu wa TEHAMA Serikalini, nchi nyingine ni Kenya, Misri, Uganda na Rwanda.

Ripoti ya GovTech Maturity Index (GTMI) 2025 imeangazia maeneo makuu manne ya TEHAMA:
Mifumo ya Mikuu ya Serikali (Core Government Systems)
Huduma Zinazotolewa Mtandaoni (Online Public Service Delivery)
Jukwaa la Ushirikishwaji Wananchi Kidijitali (Digital Citizen Engagement)
Mazingira Wezeshi (GovTech Enablers).

Mifumo ya Mikuu ya Serikali Yachochea Mafanikio
Ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa, mafanikio ya Tanzania yametokana kwa kiasi kikubwa na uwepo na matumizi ya Mifumo ya Mikuu ya Serikali (Core Government Systems).

Mifumo hiyo imejumuisha mifumo ya usimamizi wa rasilimaliwatu kama vile (Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Mishahara - ‘Human Capital Information Management System’ - HCIMS’), mifumo ya ajira (Ajira Portal), pamoja na mifumo ya kuunganisha na kubadilishana taarifa kati ya taasisi za umma (interoperability).

Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus – GovESB) umetajwa kuwa mhimili muhimu unaowezesha mifumo ya taasisi mbalimbali za umma kusomana na kubadilishana taarifa kwa usalama na ufanisi zaidi. Hatua hii imepunguza urudufu wa taarifa, kuharakisha utoaji wa huduma na kuongeza uwajibikaji.

Ushirikishwaji wa Wananchi Kidijitali

Katika eneo la Ushirikishwaji wa Wananchi Kidijitali (Digital Citizen Engagement), Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazochukua hatua madhubuti katika kujenga mifumo inayowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika masuala ya utawala.

Mfumo wa e-Mrejesho umekuwa ni nyenzo muhimu inayowaunganisha wananchi na Serikali, kwa kuwezesha utoaji wa maoni, malalamiko, ushauri na pongezi, pamoja na kupata mrejesho kwa wakati. Mfumo huu umechangia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi kwa Serikali.

Mazingira Wezeshi (GovTech Enablers)

Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao (GovTech Enablers) vimekuwa chachu ya mafanikio ya Tanzania katika mageuzi ya kidijitali.

Mazingira haya rafiki yameiwezesha Serikali kuwekeza na kusimamia miradi ya TEHAMA kwa mwelekeo mmoja wa kitaifa.

Utoaji wa Huduma Mtandaoni (Online Public Service Delivery)

Aidha, utoaji wa huduma za serikali kwa njia ya mtandao (Public Service Delivery) kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo Mkuu wa Malipo Serikalini (GePG), Mfumo wa Kitaifa wa Manunuzi ya Kielektroniki (NeST) na mifumo ya huduma za Serikali za Mitaa (TAUSI), umeongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi na kwa gharama nafuu.

Mtazamo wa e-GA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa mwelekeo sahihi wa taifa katika kujenga Serikali ya kidijitali.

“World Bank imefanya utafiti huu kwa takriban mwaka mmoja huku ikikusanya uthibitisho na taarifa mbalimbali kwenye matumizi ya TEHAMA Serikalini (Evidence-based GovTech Maturity Index Survey) katika nchi mbalimbali duniani”, amefafanua Ndomba.

Amesisitiza kuwa, uwepo wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA serikalini unaonesha usimamizi mzuri wa rasilimali za TEHAMA, na kutoa wito kwa taasisi za umma kuendelea kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa miradi ya TEHAMA. Pia amehimiza matumizi ya mifumo ya ushirikishwaji wa wananchi na kuunganisha mifumo ya taasisi na GovESB.

Mafanikio haya yanaifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mageuzi ya kidijitali barani Afrika, na kuweka msingi imara wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za umma, kukuza uwazi na kuimarisha uchumi wa kidijitali kwa maendeleo endelevu ya taifa.



Post a Comment

0 Comments