Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi
Na Paschazia Charles - Shinyanga
Maendeleo ya Jimbo la Shinyanga Mjini yamewekwa kuwa ajenda kuu ya uongozi, huku miradi mbalimbali ikiendelea kusimamiwa na kuboreshwa sekta kwa sekta ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, wakati akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga katika Ukumbi wa Ukumbi wa Lyakale, ambapo pia aliwashukuru wananchi na viongozi wa chama kwa ushirikiano wao katika kipindi cha uchaguzi.
Katambi amesema yeye pamoja na madiwani na wabunge wenzake wana wajibu wa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Mimi na viongozi wenzangu ni jukumu letu kuwaletea maendeleo na kusimamia miradi yote ya maendeleo. Niwaombe wakandarasi waliopewa dhamana ya kufanya kazi wafanye kazi kwa wakati, sitakubaliana na mkandarasi atakayesababisha ucheleweshaji bila sababu maalum,” amesema Katambi.
Amesema ushindi uliopatikana katika uchaguzi umetokana na umoja na mshikamano wa wananchi pamoja na kazi kubwa ya viongozi wa CCM katika kuhamasisha upigaji kura, akiahidi kuendeleza ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyoahidiwa.
Katika kusisitiza utawala wa haki, Katambi amesema atasimamia misingi ya kikatiba na kuhakikisha hakuna mwananchi atakayeonewa. Aidha, ameeleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila amani na utulivu, akisisitiza kuwa Shinyanga itaendelea kuwa salama kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye amani.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto za kiusalama, hususan uhalifu wa mtandaoni, ambapo wizara yake imeelekeza nguvu katika kudhibiti vitendo vya utapeli, ulaghai na upotoshaji wa taarifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewahimiza wananchi na viongozi wa chama kuendelea kumpa ushirikiano Katambi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akisisitiza umuhimu wa kuachana na majungu na kuunganisha nguvu katika kuleta maendeleo ya Shinyanga na Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, akizungumza na Viongozi wa CCM Jimbo la Shinyanga Mjini
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, akizungumza na Viongozi wa CCM Jimbo la Shinyanga Mjini
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, akizungumza na Viongozi wa CCM Jimbo la Shinyanga Mjini
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, akizungumza na Viongozi wa CCM Jimbo la Shinyanga Mjini











0 Comments