Na Mwandishi Wetu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia amesema kuwa kutotekeleza matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPA) ni hatari kwa faragha, usalama na haki za wananchi.
Hayo yalisemwa Februari 11, 2026 katika mafunzo maalum ya maafisa ulinzi wa taarifa binafsi awamu ya saba, yaliyofanyika katika ukumbi wa City Park Garden jijini Mbeya .
“Tume imebaini baadhi ya taasisi kutokua tayari kikamilifu kutekeleza matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, hususan katika usajili na uteuzi wa Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Baadhi ya taasisi zinaendelea kukusanya na kuchakata taarifa binafsi bila kukamilisha matakwa ya kisheria”
“Lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi vinafanyika kwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi. Hivyo kupitia mafunzo haya tunatarajia kuona mabadiliko ya vitendo katika taasisi zinazoshiriki mafunzo haya” amesema Dkt. Mkilia.
Dkt. Mkilia amesisitiza kuwa PDPC imejipanga kuanza ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria, kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya usajili na uteuzi wa Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na kuchukua hatua za kisheria pale ambapo kutabainika ukiukwaji.
Mafunzo hayo ya siku tatu kwa maafisa ulinzi wa taarifa binafsi yalifanyika jijini Mbeya kuanzia Februari 11, 2026 ikiwa ni awamu ya saba ya mafunzo hayo, kwa kipindi hiki yakilenga taasisi za umma na binafsi zilizopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.















0 Comments