Na Mwandishi wetu,Arusha
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameahidi Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya Utalii na miondombinu katika sekta hiyo ili kuvutia watalii zaidi.
Akizungumza katika hafla ya kutoa tuzo za Serengeti Award, jijini Arusha, Mount Meru hotel, Nchemba alisema sekta ya Utalii ina umuhimu mkubwa kwa Taifa hivyo, Mazingira ya uwekezaji yataendelea kuboreshwa na kuondolewa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Dk. Nchemba alisema Sekta ya Utalii, inachangia asilimia 21 ya pato la Taifa, ikichangia pia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni na imetoa ajira kwa watanzania zaidi ya milioni tatu.
"Hivyo serikali tunaahidi kuendelea kuilinda sekta hii kwa manufaa ya Taifa hili na tunawataka viongozi na wananchi wote kuwa walinzi wa rasilimali za taifa"alisema
Alisema katika kuhakikisha changamoto zinafanyiwa kazi Serikali itaboresha miundombinu katika maeneo kadhaa, ikiwepo ujenzi wa barabara ya Ngorongoro hadi Serengeti, uwekaji wa taa la barabara kutoka Mto wa mbu hadi Karatu.
Waziri Mkuu alitaka wizara ya maliasili na Utalii, kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, kuendelea kutatua changamoto za wizara hiyo lakini pia kuhakikisha watalii wanaongezeka na kufikia milioni 8 kwa mwaka.
Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, aliahidi wizara yake, kuendelea kushirikiana na wawekezaji na wadau wote wa sekta hiyo, ili kutimiza malengo ya serikali kukuwa kwa sekta hiyo.
Dk. Kijaji alisema pia wizara hiyo itaendelea kushirikiana na bunge na kamati yake, kuhakikisha inafikia malengo ya kukuza sekta ya Uhifadhi na Utalii na watalii kuongezeka.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika hafla hiyo, baadhi ya wawekezaji, licha ya kupongeza jitihada za serikali walitaka kutazamwa maeneo ya WMA ambao yanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaathiri sekta hiyo.
"Haya maeneo ni muhimu sana katika uhifadhi , hivyo lazima yapate viongozi wazuri ambao wanaweza kuendeleza utalii na uhifadhi badala ya sasa kuwepo na viongozi wengi ambao wamekuwa chanzo cha migogoro baina ya WMA na wawekezaji"alisema mwekezaji mmoja ambaye aliomba kuhifadhiwa jina.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mwezi mei mwaka jana ilikabidhi gawio la shilingi za kitanzania Bilioni 2.25 kwa wanufaika 51 wa shughuli za uhifadhi na utalii zikiwemo Halmashauri za Wilaya 25 kiasi cha Milioni 368, Vijiji 20 vilipewa sh Milioni 385 huku Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za jamii (WMA) sita 6 ambazo zilipatiwa kiasi cha sh Bilioni 1.5.
Serikali ilieleza kutoa gawio hilo kutokana na miongozo ya kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za utalii na kuyarudisha kwa wanufaika ikiwemo Vijiji, WMA na Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na kuongeza chachu kwa wananchi katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori.
Hata hivyo, bado kuna changamoto katika maeneo ya WMA zaidi 10 ambazo zipo nchini na sasa maeneo yao ndio yamekuwa yakitumiwa sana na wawekezaji kujenga mahoteli, kufanya utalii wa picha na Uwindaji.





0 Comments