Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPELEKA TABASAMU KWA WANAWAKE,VIJANA NA WENYE ULEMAVU MTWARA


Na Mwandishi wetu, Mtwara.

Serikali kupitia Ofisi ya  Halmashauri ya Mtwara Mikindani imekabidhi vifaa saidizi na kiasi cha shilingi milioni 342 ikiwa ni jitihada ya kujikita katika utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Mkoani Mtwara, Mkindani  leo tarehe 14/02/2026 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa sera na mwelekeo wa maendeleo unaolenga kujenga uchumi jumuishi unaowawezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa.


Naibu Waziri Ummy amefafanua, “Mikopo hii inalenga kuchochea na kuinua uchumi wa chini kwenda juu sambamba na mwelekeo wa dira ya Taifa ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.”

Ameongeza kuwa, utoaji wa vifaa saidizi ikiwemo viti mwendo, magongo, fimbo nyeupe za wasioona pamoja na taulo za kike, ni utekelezaji wa sera ya kutomwacha mtu nyuma katika safari ya maendeleo, sambamba na maono ya kitaifa ya kujenga jamii yenye heshima, utu na usawa wa fursa.


Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Dkt. Joel Arthur Nanauka, ameweka wazi kuwa Serikali katika jitahada za kuwakwamua wananchi kiuchumi itaendelea na utekelezaji wa kuleta miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mtwara ikiwemo kuboresha Bandari ya Mtwara, ujenzi wa reli, na uboreshaji wa uwanja wa ndege pamoja na marekebisho ya miundombinu ya Barabara.

Waziri Nanauka amehimiza, “Wanufaika wa mikopo hiyo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, na kurejesha kwa wakati ili kushirikiana katika kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.”


Post a Comment

0 Comments