Ticker

6/recent/ticker-posts

Dkt. Maulid Afungua Kikao Kazi cha CHAKUHAWATA, Asisitiza Ushirikiano Sekta ya Elimu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, amefungua kikao kazi cha Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu (CHAKUHAWATA) kinachofanyika jijini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wa sekta ya elimu ili kuimarisha uongozi, utawala bora na udhibiti wa ubora wa elimu nchini.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa kikao hicho, Dkt. Maulid amesema ADEM imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na jumuiya mbalimbali za elimu zikiwemo TAHOSSA, TAPSHA na REDEOA pamoja na mashirika ya kitaifa na kimataifa, kwa lengo la kuunganisha nguvu katika kufanikisha malengo ya kitaifa ya maendeleo ya elimu.

Amesema mwaliko wa kushiriki katika kikao hicho muhimu cha wadau wa sekta ya elimu umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya ADEM na CHAKUHAWATA, kwani hapo awali taasisi hizo hazikuwa na ushirikiano wa karibu katika shughuli zao.

“Taasis yetu itaitumia fursa hii na jukwaa hili muhimu kuhakikisha tunafanya kazi kwa karibu kuwajengea uwezo walimu na viongozi wa elimu nchini,” amesema Dkt. Maulid.

Aidha, ameipongeza CHAKUHAWATA kwa juhudi zake za kutekeleza majukumu yake na kwa namna inavyowasaidia wanachama wanaokumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo masuala ya ajira, majanga na ustawi wa walimu.

Dkt. Maulid amesema juhudi hizo zimechangia kukua kwa chama hicho kutoka wanachama 182 wakati wa kuanzishwa kwake mwaka 2015 hadi kufikia wanachama 49,750 kwa sasa.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha mawasiliano kati ya chama hicho na taasisi au wizara zinazowasimamia waajiri wa wanachama wao ili kujenga uelewa wa pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia za kisheria na maelewano.

Katika hatua nyingine, amewahimiza viongozi wa CHAKUHAWATA kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za wanachama na kuimarisha ushiriki wa wanachama katika vikao vya chama ili kutoa mawazo yatakayosaidia kukijenga chama kwa mujibu wa katiba yake.

Post a Comment

0 Comments