Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza ushiriki wa watoto wa kike katika masomo ya sayansi na uhandisi ili kuwapa fursa sawa katika taaluma hizo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Dkt. Mgaya ameyasema hayo wakati wa ziara ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tuliani iliyopo Magomeni walipotembelea chuoni hapo kwa lengo la kujifunza na kujionea mazingira halisi ya masomo ya sayansi na uhandisi yanavyotolewa.
Amesema chuo hicho kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kinaendelea kutekeleza mradi wa kuanzisha Kituo cha Umahiri cha masuala ya usafiri wa anga, ambacho kitakuwa na majengo pamoja na vifaa vya kisasa vinavyofanana na vile vinavyopatikana katika vyuo vikuu vya kimataifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mgaya, ziara ya wanafunzi hao imelenga kuwapa fursa ya kuona kwa vitendo mazingira ya kujifunzia pamoja na vifaa vinavyotumika katika taaluma za urubani na matengenezo ya ndege, ili kuwasaidia kupata mwamko na uelewa kuhusu fursa zilizopo nchini katika masomo ya sayansi na uhandisi.
Amefafanua kuwa takwimu zinaonesha ushiriki wa watoto wa kike katika kozi za sayansi na uhandisi bado ni mdogo, ambapo kwa sasa hauzidi asilimia 15, licha ya uwezo mkubwa wanafunzi wa kike wanaouonesha wanapopata nafasi ya kusoma masomo hayo.
Ameongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikiendesha programu mbalimbali za kuhamasisha watoto wa kike kujikita katika masomo ya sayansi, huku NIT pia ikiendelea kutembelea shule mbalimbali nchini kutoa uelewa kuhusu fursa za masomo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tuliani, Happiness Mailo, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi, hasa wa kike, kwa kuwa imewapa fursa ya kuona kwa vitendo mazingira ya masomo ya sayansi na uhandisi na hivyo kuwajengea hamasa ya kuyachagua katika masomo yao ya baadaye.
Amesema wanafunzi wengi wa kike hukata tamaa mapema kutokana na dhana potofu kuwa masomo ya sayansi ni magumu, hivyo ziara kama hizo husaidia kubadilisha mtazamo huo na kuwahamasisha kujiamini zaidi katika masomo yao.
Naye mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Tuliani, Lissa Ramadhani, amesema ziara hiyo imewasaidia kufahamu zaidi kuhusu taaluma za sayansi na uhandisi ambazo awali waliziona kuwa ngumu au zisizowahusu.
Amehimiza wanafunzi wengine wa kike kuondoa hofu na kujiamini katika kusoma masomo ya sayansi, akisema kuwa fursa za taaluma hizo ni nyingi na zina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.












0 Comments