Na Mwandishi Wetu.
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo Juni 27, 2026 limeendelea na operesheni ya kuondoa bidhaa hafifu na zisizokidhi viwango kwa kuteketeza tani 20 za bidhaa za chakula zilizokwisha muda wa matumizi (expired) na zisizokidhi matakwa ya viwango katika Dampo la Pugu Kinyamwezi, Jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo ni mwendelezo wa operesheni iliyoanza Juni 22, 2026, ambapo TBS iliteketeza tani 110 za bidhaa hafifu na zilizopigwa marufuku zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 394 katika eneo la Mbezi Gongoni, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.Katika operesheni hiyo ya awali, bidhaa zilizoteketezwa zilijumuisha tani 26 za bidhaa za mitumba ikiwemo nguo za ndani na taulo, tani 8 za vipodozi vilivyopigwa marufuku, tani 3 za bidhaa za chakula zilizokwisha muda wa matumizi pamoja na bidhaa za rangi ambazo hazikukidhi matakwa ya viwango vya ubora.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Meneja wa TBS Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, alisema bidhaa hizo hupatikana kupitia ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa katika masoko na maeneo mbalimbali ya biashara ili kulinda afya za watumiaji.Aliwataka wananchi kuendelea kuwa makini wanaponunua bidhaa kwa kusoma taarifa muhimu zilizopo kwenye vifungashio, hususan tarehe za uzalishaji na mwisho wa matumizi, na kutoa taarifa TBS wanapobaini bidhaa zenye dosari.
Aidha, TBS imesisitiza kuwa itaendelea kufanya ukaguzi nchi nzima na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kuingiza au kuuza bidhaa zisizokidhi viwango, huku ikisisitiza kuwa lengo kuu ni kulinda afya za wananchi, mazingira ya biashara na uchumi wa Taifa.












0 Comments