NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewajengea uwezo na uelewa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Bunju B kuhusu namna ya kushiriki katika huduma za ununuzi wa umma kwa kuzingatia misingi na taratibu za manunuzi ya serikali.
Zaidi ya washiriki 100 walishiriki mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika Machi 14, 2026, Bunju B jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Kuendeleza Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Girbert Kamnde, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea washiriki uwezo na uelewa kuhusu utaratibu wa ununuzi wa umma, hususan nafasi ya asilimia 30 iliyotengwa kwa makundi maalumu.
Kamnde amesema katika mafunzo hayo washiriki wanaelekezwa namna mfumo wa ununuzi wa umma unavyotekelezwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NEST), ikiwa ni pamoja na namna ya kujisajili kwenye mfumo huo, kuhuisha taarifa zao pamoja na kuomba zabuni kupitia mfumo huo.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la KKKT Bunju B, Kingdom Mbangula, amesema semina hiyo imekuwa yenye manufaa makubwa kwa waumini kwani PPRA imewafikia kwa urahisi na kuwapatia mafunzo muhimu yatakayowasaidia kushiriki katika fursa za manunuzi ya serikali.
“Mafunzo haya yatakuwa na manufaa makubwa katika maisha yetu kwa sababu kupitia elimu hii vikundi vyetu vitapata nafasi ya kuingia katika mifumo ya kiserikali, hususan mfumo wa manunuzi wa PPRA,” amesema Mbangula.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa KKKT Bunju B, Mwinjilisti Esther Ngondya, ameishukuru PPRA kwa kuwafikia na kuwapatia elimu kuhusu masuala ya ununuzi wa umma, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa vikundi vyao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, muumini wa kanisa hilo aliyeshiriki mafunzo hayo, Josephine Mfaume, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa kuwa kila mwananchi ana haki ya kushiriki katika manunuzi ya serikali na kuomba zabuni za serikali.











0 Comments