Ticker

6/recent/ticker-posts

MAONESHO YA SIDO KITAIFA KUFANYIKA MKOANI SHINYANGA

Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) limetangaza kuwa Maonesho yake ya Tano ya Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Oktoba 21 hadi 30, 2026 katika Uwanja wa Magufuli uliopo Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, yakilenga kuinua uchumi wa wajasiriamali wadogo nchini.

Akizungumza Aprili 10, 2026 na wajasiriamali kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Silvester Mpanduji amesema tukio hilo litatoa fursa ya kujifunza mbinu bora za uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na ushindani, pamoja na kupanua mitandao ya kibiashara.

Amesema maonesho hayo yatawakutanisha wajasiriamali, taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.

“Maonesho haya yatakuwa jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kujitangaza, kupanua masoko, na kujifunza mbinu bora za uzalishaji,” amesema Prof. Mpanduji.

Kwa mujibu wa SIDO, zaidi ya wajasiriamali 600 kutoka Tanzania Bara na Visiwani wanatarajiwa kushiriki, sambamba na taasisi zaidi ya 50 zinazotoa huduma kwa sekta ya viwanda vidogo na vya kati.

Mbali na hilo, washiriki watapata fursa ya kujenga mitandao ya kibiashara, kukutana na wanunuzi na wawekezaji wapya, pamoja na kupata mitaji kupitia taasisi za kifedha.

Aidha, wananchi watapata nafasi ya kujifunza kuhusu bidhaa zinazozalishwa nchini na teknolojia mbalimbali zinazoweza kusaidia kuanzisha viwanda vidogo.

SIDO imewahamasisha wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili kunufaika na fursa za kibiashara, huku sekta binafsi ikihimizwa kudhamini na kuonesha huduma zao.

Wananchi, hususan vijana na wanawake, wametakiwa kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kujifunza namna ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Kwa ujumla, maonesho ya SIDO yameendelea kuwa chachu muhimu ya kukuza uchumi wa viwanda nchini kwa kuhamasisha ubunifu, ushindani na upatikanaji wa masoko kwa wazalishaji wa ndani.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi amesema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Ameeleza kuwa miundombinu ya usafiri, huduma za malazi pamoja na ulinzi na usalama viko katika hali nzuri kwa ajili ya kuhudumia wageni na washiriki.

“Mkoa wa Shinyanga upo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha maonesho haya yanafanikiwa na kuleta tija kwa washiriki na wananchi kwa ujumla,” amesema Lyamongi.

Aidha, Uwanja wa Magufuli uliopo Kahama umetajwa kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya maonesho hayo kutokana na ukubwa wake na urahisi wa kufikika kutoka maeneo mbalimbali ya nchi

Post a Comment

0 Comments