Ticker

6/recent/ticker-posts

Waziri Kombo Ashiriki Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi Mauritius

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameshiriki Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi, unaofanyika jijini Port Louis, Mauritius Aprili 10 hadi 12, 2026.

Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wataalamu wa masuala ya usalama wa bahari, pamoja na wadau wa maendeleo kutoka mataifa yanayozunguka Bahari ya Hindi kujadili fursa na changamoto zinazohusiana na usalama wa bahari, biashara, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na ushirikiano wa kiuchumi katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Mkutano huo umefunguliwa na Waziri Mkuu wa Mauritius Mheshimiwa Dr. Navinchandra Ramgoolam aliyesisitiza umoja, ushirikiano, na uwajibikaji wa pamoja miongoni mwa mataifa ya Bahari ya Hindi. Ametoa wito kwa nchi kushirikiana kukabiliana na changamoto za pamoja kama vile vitisho vya usalama, mabadiliko ya tabianchi, na maendeleo ya kiuchumi, ili kujenga mustakabali salama, endelevu, na wenye ustawi kwa eneo hilo.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mheshimiwa Subrahmanyam Jaishankar amesisitiza umuhimu wa ushirikiano imara wa kikanda na uwajibikaji wa pamoja katika Bahari ya Hindi. Alithibitisha dhamira ya India ya kukuza utulivu, maendeleo, ustawi na kuhimiza nchi za bahari ya Hindi kushirikiana katika kukabiliana na changamoto kuu kama usalama wa baharini, mabadiliko ya tabianchi, na maendeleo endelevu ili kuhakikisha eneo lenye amani na ustahimilivu.

Wakati wa Mkutano huo Mhe. Waziri Kombo atashiriki mijadala ya ngazi ya juu, kuelezea umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na uchumi wa buluu. Balozi Kombo pia atafanya mazungumzo ya pande mbili na mawaziri na viongozi kutoka nchi mbalimbali ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi hizo.

Mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo, uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja itakayochochea maendeleo endelevu kwa mataifa yanayozunguka Bahari ya Hindi na dunia kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments