
Wadau wa mazingira wilayani Mbinga wameunda kamati za mazingira na maji ili kulinda uhifadhi mazingira na kuhifadhi maji katika bonde la mto Ruvuma.
Kuundwa kwa kamati hizo kumekuja baada ya mafunzo yaliyofanywa na shirika la Youth Environmental Justice and Gender Equality (YOGE) na Tanzania Media for Community Development, kwa ufadhili wa IUCN’s BRIDGE Women Leadership Grants.
Mafunzo hayo yalifanywa chini ya mradi wa Sauti za maji unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika ngazi za maamuzi ili kuhifadhi rasilimali maji na mazingira kwenye bonde la mto Ruvuma.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Makori alisisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada za kutunza mazingira ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Makori
Alipongeza shirika la YOGE kwa kupeleka mradi huo wilayani humo na kusema kuwa kufanya hivyo kunachagiza jitihada za Serikali za kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambacho kwa sasa ni kipaumbele cha taifa.
Awali, Mkurugenzi wa YOGE Wakili Philomena Mwalongo alisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kuhifadhi rasilimali maji kwani kushindwa kufanya hivyo kunaweza kufanya bidhaa hiyo ikawa ghali.
Wakili Philomena Mwalongo
Alitoa mfano wa Dar es Salaam ambapo wakati mwingine kumekuwa na upungufu wa maji kutokana na kina cha Mto Ruvu kupungua na kusisitiza kuwa ni vema kuzuia hali hiyo isijitokeze katika bonde la mto Ruvuma.
Mafunzo hayo yalishirikisha wadau mbalimbali wa mazingira wakiwemo viongozi wa kimila, dini, asasi za kiraia, mamlaka za maji, vijana na wanawake, watendaji katika wilaya ya Mbinga.
Wilaya ya Mbinga almaarufu kama Mbinguni imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba na kahawa inayonukia na yenye radha tamu.
Wilaya hiyo ina fursa nyingi za chakula na biashara na hali ya hewa nzuri na vivutio mbalimbali pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji.


































0 Comments