Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. SHEMDOE AMSHUKURU MHE. RAIS SAMIA KUTOA FEDHA ZA KUTEKELEZA MIRADI KWENYE MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

 

Na OWM - TAMISEMI, Arusha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia fedha nyingi kupelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imepeleka tabasamu kwa wananchi kwa kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.

Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo Aprili 22, 2026 jijini Arusha kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kufungua Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika tarehe 22 hadi 23 Aprili, 2026 jijini humo.

“Mhe. Waziri Mkuu, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mhe. Rais kwa kuleta fedha nyingi  katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zimetekeleza miradi mingi ya kimkakati, nakushukuru nawe pia kwani ukiwa Waziri wa Fedha uliwezesha upatikanaji wa fedha zote zilizoridhiwa na Mhe. Rais,” amesisitiza Mhe. Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amewapongeza Wastahiki Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri kwa kuchaguliwa na mabaraza yao kuwaongoza Waheshimiwa Madiwani, na kuwataka kuilinda imani waliyopewa na wananchi kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa katika kuwatumikia wananchi.

Aidha, Prof. Shemdoe amewapongeza pia Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kwa kufanya kazi kubwa ya usimamizi wa miradi pamoja na rasilimaliwatu, hatua iliyowezesha kufikia ndoto ya Mhe. Rais ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawaletea tabasamu la kudumu wananchi walioko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Post a Comment

0 Comments