Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza matumizi ya mafuta kwa kutumia magari machache kwenye ziara za kikazi, huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwa kutumia gari moja katika ziara ya kikazi wilayani Bahi.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Aprili 17, 2026 wakati wa kikao chake na viongozi wa mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Bahi kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi, kabla ya kuongoza hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili na kidato cha nne iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Chiona wilayani Bahi.
“Wakuu wa Mikoa na Wilaya muendelee kupunguza misafara yenu mnapokuwa kwenye ziara za kikazi kama ambavyo mmeona juzi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo, hivyo naelekeza mpunguze matumizi ya mafuta kwa kutumia magari machache iwezekanavyo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesema kuwa, ana imani kwamba Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote watatekeleza maelekezo ya kupunguza gharama za matumizi ya mafuta kwa kutumia gari moja kama alivyofanya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo, hususani katika kipindi hiki ambacho mafuta yamepanda bei na kuathiri uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Prof. Shemdoe ameendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza na kusimamia utekelezaji wa Maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa, ambayo wamekuwa wakiyatoa kwa mustakabali na masilahi mapana ya maendeleo ya taifa, likiwepo hili la kuondoa gharama kubwa za matumizi ya kununua mafuta kwa kupunguza idadi ya magari kwenye misafara ya viongozi wa mikoa na wilaya.









0 Comments