Ticker

6/recent/ticker-posts

SEKTA YA MATUKIO YACHANGIA KUKUA KWA UCHUMI JUMUISHI NCHINI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Serikali imeendelea kuitambua sekta ya matukio na biashara za sherehe kama kichocheo muhimu cha ajira na ukuaji wa uchumi nchini, huku ikiwahimiza vijana na wanawake kuitumia kama jukwaa la kujiajiri na kuongeza kipato.

Akizungumza katika kilele cha Maonesho ya Wafanyabiashara wa Sherehe (Adorable Wedding Trade Fair – Msimu wa Nane), Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema sekta ya sherehe inazalisha ajira kwa maelfu ya Watanzania, hususan vijana na wanawake, huku ikiunganisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo utalii, usafirishaji, mavazi, chakula na teknolojia ya ubunifu.

“Sekta hii si burudani tu bali ni injini ya uchumi. Inachochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati na kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi,” amesema Kapinga.

Aidha, Waziri huyo amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni vijana, hali inayofanya sekta hiyo kuwa fursa muhimu ya ajira inayohitaji mtaji mdogo. Alitaja maeneo yenye fursa kubwa kuwa ni upigaji picha, mapambo ya matukio, upangaji wa sherehe, upishi, matumizi ya mitandao ya kijamii, ubunifu wa mavazi na burudani.

Kapinga amewahimiza vijana kuacha kusubiri ajira rasmi na badala yake kutumia ubunifu na teknolojia kuanzisha biashara zao, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kupitia mafunzo, mitaji na sera zinazounga mkono ujasiriamali.

Pia ameeleza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kurahisisha mifumo ya usajili, kukuza matumizi ya teknolojia na kuwezesha upatikanaji wa mitaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amewataka wadau wa sekta hiyo kuzingatia ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia ya kidijitali, ushirikiano wa kibiashara na urasimishaji wa shughuli zao ili kunufaika na fursa za ndani na kimataifa.

Awali, amempongeza muandaaji wa maonesho hayo, Anna Lema, kwa kuendelea kukuza jukwaa hilo linalowakutanisha wadau wa sekta ya sherehe na kutoa fursa kwa wajasiriamali chipukizi.

Maonesho hayo yaliyoambatana na kaulimbiu ya “Craft Your Moment” yamehusisha washiriki zaidi ya 100, wakiwemo wanavyuo walioshiriki katika mashindano ya ubunifu na ujasiriamali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi na Muandaaji wa Adorable Wedding Trade Fair, Anna Lema amesema kupitia jukwaa la Adorable Wedding Trade Fair wamefanikiwa kuongeza ubora wa huduma, kujenga ushindani chanya na kuinua viwango vya matukio nchini kufikia hadhi ya kimataifa.

“Sekta ya matukio ni pana na ina ajira nyingi. Mpambaji mmoja anaweza kuajiri watu 15 hadi 20, huku ukumbi wa sherehe ukitoa ajira kwa zaidi ya watu 30. Hii inaonesha wazi mchango wake katika uchumi,” amesema.

Ameziomba mamlaka husika kuhakikisha sekta hiyo inatambuliwa na kuwezeshwa zaidi ili iweze kukua na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Katika kuimarisha mchango wa kijamii, amesema maonesho hayo yameendelea kugusa jamii kupitia programu ya “Lucky Couple Lottery Coupon” inayowezesha baadhi ya wanandoa kufanyiwa harusi kwa udhamini mkubwa, ambapo mwaka huu washindi wanatarajiwa kupata punguzo la hadi asilimia 70 ya gharama za huduma za harusi.

Aidha, kwa mara ya kwanza waandaaji wameanzisha mashindano ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, Adorable University Student Entrepreneurship Competition, yaliyopokea zaidi ya mawazo 107 ya biashara.

Mshindi wa mashindano hayo atajishindia Sh milioni mbili pamoja na fursa ya mafunzo elekezi (mentorship) ili kukuza wazo lake la biashara.

Post a Comment

0 Comments