Serikali imepanga kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa mafunzo na uendelezaji wa watumishi wa umma kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma bora na kuongeza ufanisi serikalini.
Akizungumza leo Aprili 17, 2026 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Nchi katika ofisi hiyo, Ridhiwani Kikwete, alisema serikali imejipanga kuboresha mafunzo ya watumishi ili kuendana na mahitaji ya utendaji wa kisasa.
Alisema TPSC itaendeleza na kuboresha programu mpya 15 za mafunzo zitakazolenga maeneo ya uongozi, usimamizi na utawala, kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi na tija zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, jumla ya watumishi 10,000 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya kujiandaa na mitihani ya utumishi wa umma, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi na ubora wa utendaji kazi serikalini. Aidha, watumishi wengine 20,000 watapatiwa mafunzo ya uongozi, menejimenti na usimamizi wa ofisi, huku watumishi 3,000 wakipata mafunzo hayo kupitia mifumo ya mtandao.
Katika hatua nyingine, watumishi wapya 10,000 watanufaika na mafunzo ya awali yatakayowajengea uelewa wa mifumo ya serikali na misingi ya utumishi wa umma, ikiwa ni maandalizi muhimu ya kuwasaidia kuanza majukumu yao kwa ufanisi.
Akizungumzia matumizi ya teknolojia, Kikwete alisema chuo hicho kitaboreshwa kwa kuongeza miundombinu ya ujifunzaji wa kidijitali ili kupanua wigo wa upatikanaji wa mafunzo kwa watumishi wengi zaidi kwa gharama nafuu bila kuathiri ubora wa mafunzo hayo.
Kwa upande wa mafunzo ya muda mrefu, alisema washiriki 13,400 watapatiwa elimu katika fani mbalimbali ikiwemo utunzaji wa kumbukumbu, uhazili, TEHAMA, usimamizi wa fedha za umma, rasilimaliwatu, manunuzi ya umma pamoja na uongozi na utawala bora.
Mbali na mafunzo, TPSC pia inatarajia kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa taasisi 12 za umma kwa lengo la kubaini changamoto za kiutendaji na kutoa mapendekezo ya maboresho yatakayoongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Sambamba na hilo, tafiti tumizi 14 pamoja na machapisho 20 yatafanyika ili kusaidia maboresho ya sera na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hatua hizo zinaakisi dhamira ya serikali ya kuimarisha rasilimaliwatu katika sekta ya umma na kuhakikisha watumishi wanakuwa na ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya wakati, hivyo kuongeza tija na uwajibikaji katika utumishi wa umma.


0 Comments