NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Katika jitihada za kimataifa za kudhibiti matumizi ya plastiki na kupunguza athari zake kwa afya ya binadamu na mazingira, wadau mbalimbali wameendelea kushiriki kikamilifu katika mjadala wa mkataba wa kimataifa wa plastiki unaoendelea kujadiliwa.
Lengo kuu la mchakato huo ni kubaini changamoto zilizopo, kuziba mapengo ya kisheria, na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali hatarishi zinazotumika katika uzalishaji wa plastiki.
Akizungumza katika warsha ya wadau iliyofanyika Aprili 14, 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Programu Mkuu kutoka Agenda for Environment and Responsible Development, Silvani Mng’anya, alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika kuhakikisha mkataba huo unakuwa na tija kwa Tanzania na dunia kwa ujumla.
Alieleza kuwa warsha hiyo imelenga kukusanya maoni na taarifa zitakazosaidia kuandaa msimamo wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo inaratibu ushiriki wa nchi katika majadiliano hayo ya kimataifa.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa mkataba huu unazingatia kwa kina suala la kemikali hatarishi zinazopatikana katika plastiki, hasa zile zinazotumika katika vifungashio vya vyakula na vinywaji, ambazo zinaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira,” alisema.
Aliongeza kuwa tafiti mbalimbali zimebaini uwepo wa kemikali kama Bisphenol A (BPA) na phthalates katika baadhi ya bidhaa za plastiki, ambazo zinaweza kuathiri mfumo wa homoni mwilini na kusababisha matatizo ya kiafya.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo, Dorah Swai, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote wakiwemo serikali, wazalishaji wa viwandani, na mashirika ya kiraia katika kuhakikisha plastiki zinazozalishwa zinakuwa salama na hazina kemikali hatarishi.
Aidha, alieleza kuwa ni muhimu kuanza kushughulikia tatizo hilo kuanzia kwenye chanzo cha uzalishaji badala ya kusubiri madhara baada ya bidhaa kuingia sokoni.
“Katika taaluma ya mazingira, tunasisitizwa kuwa suluhisho la matatizo ya mazingira lianzie kwenye chanzo. Hatuwezi kuendelea kuzalisha bidhaa zenye kemikali hatarishi halafu baadaye tukajaribu kuzidhibiti au kuziteketeza,” alifafanua.
Washiriki wa warsha hiyo walipata fursa ya kujadili kwa kina namna kemikali hizo zinavyoingia katika mnyororo wa uzalishaji wa plastiki na athari zake kwa afya ya binadamu, hususan kupitia matumizi ya kila siku ya vifungashio vya chakula na vinywaji.
Naye Theophil Andrew kutoka PETpro-Tanzania alisisitiza haja ya kuwepo kwa sera na sheria madhubuti zitakazodhibiti matumizi ya kemikali hizo, pamoja na kuhimiza matumizi ya teknolojia mbadala salama katika uzalishaji wa plastiki.
Amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kutoa mchango wenye tija katika majadiliano ya mkataba wa kimataifa wa plastiki unaolenga kupunguza athari za plastiki na kulinda afya za binadamu pamoja na mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
0 Comments