Ticker

6/recent/ticker-posts

DK.MWINYI - CCM ITAENDELEA KUJIIMARISHA KIUCHUMI

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi amesema atahakikisha maeneo yote yenye hadhi ya uwekezaji ndani ya Chama yanatafutiwa wawekezaji wakubwa watakaoweza kusimamisha miradi yenye tija kiuchumi ndani ya CCM na Jumuiya zake.

Dk. Mwinyi alisema wakati umefika kwa CCM kufanya mapinduzi ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali zake ipasavyo, akieleza kuwa licha ya Chama kuwa na mali na maeneo mengi ya uwekezaji, bado havizalishi mapato yanayolingana na thamani yake halisi.

Kauli hiyo aliitoa wakati akihitimisha ziara yake ya kuimarisha Chama upande wa Unguja alipokutana na viongozi wa Halmashauri Kuu za CCM Mkoa wa Magharib, Wilaya ya Mfenesini na Wilaya ya Dimani katika mkutano uliofanyika Bweleo, Unguja.

Alisema CCM inapaswa kuelekeza nguvu katika uwekezaji wa miradi mikubwa yenye kuingiza mapato makubwa ikiwemo majengo ya kisasa ya biashara, nyumba za kupangisha na kuuza, kumbi za mikutano za kimataifa pamoja na mahoteli ya hadhi ya juu.

Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa kila ngazi ya uongozi ndani ya Chama na Jumuiya zake kuanzia matawi hadi mikoa inapaswa kubadili mtazamo wa uwekezaji mdogo mdogo ambao hauna tija kubwa katika kukuza uchumi wa Chama.

“Ndugu viongozi wenzangu, Chama chetu kinahitaji kukua kiuchumi kwa sababu tunahitaji fedha za kuendesha shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ofisi za kisasa, posho na mishahara ya watumishi, ununuzi wa magari pamoja na vifaa vya ofisi. Hivyo ni muhimu kutumia vizuri rasilimali tulizonazo kwa manufaa ya Chama,” alisema Dk. Mwinyi.

Aliongeza kuwa miradi midogo yenye mapato ya kodi ya Shilingi 100,000 au 200,000 kwa mwezi haiwezi kusaidia kufikia malengo makubwa ya kiuchumi ya Chama, hivyo kuna haja ya kuelekeza nguvu katika miradi mikubwa yenye mapato makubwa na endelevu.

Aidha, alisema CCM haijawahi kufanya mikutano yake mikuu Zanzibar, lakini kwa mipango ya uwekezaji wa miundombinu ya kisasa ikiwemo ukumbi mkubwa wa mikutano, Zanzibar itaweza kuwa mwenyeji wa mikutano hiyo katika miaka ijayo.

Dk. Mwinyi alisema utekelezaji wa malengo hayo utaifanya CCM kwenda sambamba na vyama vikubwa vya ukombozi na kijamaa duniani ambavyo vina uchumi imara kupitia uwekezaji wa miradi mbalimbali.

Katika mkutano huo pia alizungumzia suala la fidia kwa baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Dimani walioathiriwa na ujenzi wa barabara, akieleza kuwa Serikali itahakikisha kila mwenye haki analipwa stahiki zake, huku waliopokea fedha kwa njia za udanganyifu wakitakiwa kuzirejesha ili waliostahili walipwe.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohamed Said Dimwa aliwapongeza viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Magharib kwa kuendelea kukisimamia Chama kwa mshikamano, nidhamu na uaminifu.

Dk. Dimwa alisema CCM imejipanga kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Chama wa mwaka 2027 unafanyika kwa misingi ya demokrasia, nidhamu na mshikamano, huku akiwataka wanachama kuepuka makundi na kuendeleza siasa safi zinazolinda umoja wa Chama.

Aliongeza kuwa CCM tayari imeanza kujiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa dola wa mwaka 2030 kwa kuandaa viongozi wenye uwezo, maadili na uzalendo ili kuendelea kuaminiwa na wananchi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharib, Mohamed Rajab Soud alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuimarisha miradi ya maendeleo katika sekta za afya, kilimo, elimu, maji na miundombinu ya barabara pamoja na ujenzi wa kiwanja cha kisasa kitakachotumika katika mashindano ya AFCON 2027, akisema hatua hiyo itaendelea kuitangaza Zanzibar kimataifa.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, akiwahutubia Viongozi na Wanachama wa CCM Mkoa wa Magharib wakati akihitimisha ziara zake katika Mkoa huo kwa upande wa Unguja huko Bweleo Unguja.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akitoa salamu za CCM katika ziara ya kichama ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi iliyofanyika Mkoa wa Magharib huko Bweleo Unguja.
BAADHI ya Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wakifuatilia hotuba na nasaha za Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi wakati akizungumza katika ziara yake Mkoa wa Magharib Unguja.

Post a Comment

0 Comments