Ticker

6/recent/ticker-posts

HAKUNA NYONGEZA YA MUDA KWA MKANDARASI WA UJENZI WA BARABARA KAHAMA KUPITIA MRADI WA TACTIC - PROF. SHEMDOE

 

Na OWM - TAMISEMI, Kahama

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali haitomuongezea muda Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation wa kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara na mitaro katika Manispaa ya Kahama, inayotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kwani ubovu wa miundombinu ya barabara imekuwa ni kero ya muda mrefu kwa wananchi wa manispaa hiyo.

Prof. Shemdoe amesema hayo leo Mei 27, 2026 Katika Manispaa ya Kahama wakati wa hafla ya Utiaji Saini wa Mkataba wa Umaliziaji wa Ujenzi wa Barabara na Mitaro kupitia Mradi wa TACTIC, iliyofanyika katika eneo la Phantom kwenye manispaa hiyo.  

“Ninamueelekeza Mkandarasi Kampuni ya M/s China Civil Engineering Construction Corporation kumaliza ujenzi ndani ya muda ulioanishwa katika mkataba ambao wameusaini leo, hakutakuwa na nyongeza ya muda,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amemtaka Mtaalamu Mshauri kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama  pamoja na TARURA katika kuhakikisha mikataba iliyosainiwa inatekelezwa kikamilifu na  inakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa ubora uliokubalika ili thamani ya fedha ionekane.

Prof. Shemdoe ameanisha kuwa Mei 27, 2026 imekuwa ni siku yenye furaha kwani kitendo cha kusainiwa kwa mikataba hiyo kinasadifu nia ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaboreshea miundombinu ya barabara wananchi wa Kahama, na kuongeza kuwa kama lilivyo jina lake amekuwa ni suluhu ya changamoto iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Manispaa ya Kahama.

“Tumeshuhudia utiaji saini wa mradi huu mkubwa wa zaidi ya Shilingi Bilioni 25 ambazo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia zitumike kujenga miundombinu ya barabara katika Manispaa ya Kahama, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2025 hivyo tunamshukuru sana na kumuahidi kwamba ofisi yangu itasasimamia kikamilifu utekelezaji wa mkataba huo,” amesema Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita amesema Manispaa ya Kahama inatekeleza mradi wa TACTIC kwa awamu mbili, awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara za katikati ya mji (Central Business District (CBD) zenye urefu wa Kilomita 12.3 na barabara ya eneo la Zongomela kilomita tatu (3)  pamoja na ujenzi wa  mfereji wa maji ya mvua wa Chelsea – Lyazungu,  Shunu – Magobeko (Standalone Storm Water Drain).

Mhe. Mhita amesema kwamba, awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa TACTIC katika Manispaa ya Kahama utahusisha ujenzi wa kituo cha mabasi Mbulu (Mbulu Bus Terminal), Soko la Sango (Sango Market) na Kituo kidogo cha mabasi cha Zongomela (Zongomela Mini Bus Stand).

Naye, Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano na Benki ya Dunia  Mhandisi Humprey Kanyenye wa TARURA amesema kuwa, Mkandarasi  ambaye ni Kampuni ya M/s China Civil Engineering Construction Corporation anakwenda kutekeleza mradi huu katika Manispaa ya Kahama kwa gharama ya Shilingi za kitanzania Bilioni  25,547,162,432.04 bila VAT, na utatekelezwa kwa muda wa miezi nane (8) kuanzia  Juni 01, 2026 hadi Januari 31, 2027.














Post a Comment

0 Comments