Na Farida Mangube Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanza utekelezaji wa miradi mipya 12 ya utafiti yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 3.4 kwa lengo la kukuza maarifa na kutatua changamoto katika sekta za kilimo, mifugo, mazingira na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Profesa Raphael Chibunda, wakati wa mahafali ya 47 ya chuo hicho ambapo jumla ya wahitimu 877 walitunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba.
Profesa Chibunda amesema kuanza kwa miradi hiyo kumefanya chuo hicho kufikisha jumla ya miradi ya utafiti 130 inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Chuo kinaendelea kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti zetu katika kuchangia sera na mipango ya taifa. Katika kipindi hiki cha taarifa, chuo kimeanza utekelezaji wa miradi mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4,” alisema Profesa Chibunda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha SUA, Andrew Masawe, alisema baraza hilo limeendelea kutekeleza kwa kiwango kikubwa mikakati ya kuboresha sura ya chuo, ikiwemo kusimamia matumizi bora ya fedha na ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema baraza limeendelea kuhimiza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya chuo kupitia mapato ya ndani, ambapo utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea kwa ufanisi mkubwa.
“Baraza limeendelea kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo kiasi cha shilingi bilioni 59.6 kimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Masawe.
Naye Kelvin Gwabala, mhitimu wa Shahada ya Umahiri wa Habari na Menejimenti ya Maarifa, alisema tafiti zinazofanywa na wataalamu wa SUA zimekuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan wakulima.
Alisema katika utafiti wake alibaini umuhimu wa matumizi ya vyombo vya habari katika kuchangia ukuaji na ongezeko la mavuno kwa wakulima, hasa kupitia vipindi vya kilimo vinavyorushwa na redio ya chuo hicho, SUA FM.
“Ni muhimu serikali na jamii kutumia matokeo ya tafiti zinazofanywa na watafiti. Tafiti hizi zinapowafikia wakulima moja kwa moja, matokeo yake huonekana kwa muda mfupi kupitia ongezeko la mavuno. Mfano, mkulima aliyekuwa akivuna magunia 10 anaweza kufikia kuvuna magunia 30 hadi 40,” alisema Gwabala.








0 Comments