Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Jumanne Wagana akikabidhi msaada wa madawati 40 shule ya msingi Tindeng'hulu Halmashauri ya Shinyanga
Na Stella Herman, Shinyanga
Benki ya CRDB imeendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha mazingira ya elimu kwa kutoa msaada wa madawati 40 kwa Shule ya msingi Tindeng'hulu iliyopo Kata ya Usule, Wilaya ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni yake ya “Keti Jifunze” inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati hayo Juni 1, 2026, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, amesema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa Benki hiyo wa kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amesema madawati hayo yatachangia kuondoa changamoto ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini, jambo litakaloongeza ari ya kujifunza, kuboresha usikivu darasani na kuwawezesha walimu kufundisha katika mazingira bora zaidi.
“Tunashiriki katika kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, mazingira na maeneo mengine ya kijamii, Tunatambua kuwa Serikali ina majukumu mengi ya kuhudumia wananchi, hivyo sisi kama wadau wa maendeleo tunaona ni muhimu kutoa mchango wetu katika kupunguza changamoto zilizopo,” amesema Wagana.
Aidha, amewaomba wananchi kuendelea kutumia huduma za Benki ya CRDB ili kuongeza uwezo wa Benki hiyo kuendelea kurejesha sehemu ya mapato yake kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo.
“Ninawaomba muendelee kutumia huduma za Benki ya CRDB kadri matumizi ya huduma zetu yanavyoongezeka, ndivyo tunavyopata uwezo mkubwa zaidi wa kuendelea kusaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo,”amesema Wagana
Wagana amesema kuwa Benki ya CRDB inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kifedha zikiwemo mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara, huku akisisitiza kuwa benki hiyo ipo kwa ajili ya Watanzania wote na ina jukumu la kusaidia ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Jumanne Wagana.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Said Kitinga, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii kupitia miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga.
Amesema msaada huo ni mfano wa ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii, hususan elimu.
Kitinga amewataka wanafunzi kuyatunza madawati hayo kwa kuepuka kuyaharibu kupitia matumizi yasiyo sahihi, ikiwemo kuruka juu yake, huku akisisitiza umuhimu wa kuyafanyia matengenezo madawati yanayoharibika ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Sethi Msangwa, amesema tatizo la upungufu wa madawati bado ni changamoto katika baadhi ya shule za halmashauri hiyo, hivyo msaada wa Benki ya CRDB umekuja kwa wakati muafaka na umechangia kupunguza tatizo hilo.
Amebainisha kuwa ushirikiano wa wadau wa maendeleo kama Benki ya CRDB ni muhimu katika kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga akizungumza kwenye hafla hiyo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga Sethi Msangwa akitoa shukrani kwa Benki ya CRDB kwa msaada wa madawati
0 Comments