Ticker

6/recent/ticker-posts

DOYO AWATAKA WANASIASA WAACHE MBIO ZA MAPEMA ZA URAIS



Na Oscar Assenga,TANGA

KATIBU Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amewataka baadhi ya wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 kuelekeza nguvu zao katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi badala ya kuanza harakati za kisiasa mapema.

Akizungumza jijini Tanga mara baada ya kuhitimisha ziara ya kichama mkoani humo, Doyo alisema taifa kwa sasa linahitaji mjadala unaolenga maendeleo, ustawi wa wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuliko mijadala ya urais ambayo muda wake bado haujafika.

Alisema kuwa ingawa Katiba na sheria za nchi zinatoa haki kwa kila mwananchi mwenye sifa kugombea nafasi yoyote ya uongozi, ikiwemo urais, si jambo la busara kwa viongozi kuanza kujinadi kisiasa wakati wananchi bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo.


“Ni haki yao kikatiba na kisheria kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Hata hivyo, kwa mtazamo wetu, si jambo lenye afya kwa taifa kuanza mijadala ya urais miezi michache tu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika,” alisema Doyo.

Doyo alidai kuwa katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge wa CCM wamekuwa wakitoa kauli ndani ya Bunge na kwenye mikutano ya hadhara ambazo, kwa tafsiri yake, zinaashiria kuanza kwa harakati za kuwania urais wa mwaka 2030.

Alisema viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wanapaswa kutumia nafasi zao kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuibua hoja zenye tija na kuishauri serikali katika masuala yatakayoboresha maisha ya Watanzania.


“Wananchi waliwachagua wabunge wao kwa matarajio ya kuona changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi. Tungetarajia kuona nguvu nyingi zikielekezwa katika kujadili maendeleo, uchumi, huduma za jamii na ustawi wa wananchi kuliko kujenga mazingira ya kampeni za uchaguzi ambao bado uko mbali,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Doyo, kuanza kwa siasa za urais mapema kunaweza kuathiri umakini wa viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao na kupunguza kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha, aligusia kauli mbalimbali zilizowahi kutolewa na baadhi ya viongozi wa serikali kuhusu watu wanaotamani nafasi ya urais mapema, akisema hali hiyo inaonyesha dalili za kuanza kujitokeza kwa makundi ya kisiasa ndani ya chama tawala kabla ya wakati wake.

Pamoja na hayo, Doyo alisisitiza kuwa viongozi wa vyama vyote vya siasa wanapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kushirikiana kutafuta suluhisho la changamoto zinazowagusa wananchi katika maisha yao ya kila siku.
Atoa Wito wa Kumuunga Mkono Rais Samia

Katika hatua nyingine, Doyo aliwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kusimamia maendeleo ya nchi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.


“Sasa ni wakati wa kushughulikia changamoto za wananchi, kuimarisha huduma za kijamii na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya taifa. Wakati wa siasa za urais ukifika, kila mwenye sifa na nia atapata nafasi ya kujitokeza,” alisema.

Post a Comment

0 Comments