Jukwaa la Uunganishaji wa Masoko (Market Linkage Forum) lililoandaliwa na Hand in Hand Eastern Africa Tanzania limefanyika Juni 16, 2026 katika Ukumbi wa Social Hall mkoani Singida, likiwa na lengo la kuwaunganisha wanufaika wake na wanunuzi mbalimbali ili kuimarisha upatikanaji wa masoko na kukuza biashara zao.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Meneja wa Mnyororo wa Thamani, Lucas Michael, alisema sekta ya ufugaji wa kuku ni fursa muhimu ya kuongeza kipato na kuboresha maisha ya wananchi kupitia mnyororo wa thamani wa uzalishaji na biashara ya kuku.
Kwa upande wake, Mkuu wa Tawi la Manyara wa Hand in Hand Eastern Africa Tanzania, Yona Ona, alisema jukwaa hilo linalenga kutatua changamoto ya ukosefu wa masoko kwa kuwaunganisha wanufaika wa shirika hilo na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali.
Aidha, alieleza kuwa jukwaa hilo ni mwanzo wa majukwaa mengine yatakayowaleta pamoja wazalishaji na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wanufaika wa Hand in Hand, hatua itakayochochea upanuzi wa fursa za masoko na ukuaji wa biashara.
Jukwaa hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kujifunza, kujenga mitandao ya kibiashara na kuimarisha mahusiano yatakayochangia ukuaji wa biashara na maendeleo ya sekta za uzalishaji.




0 Comments