Ticker

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU 2026 WARIDHISHWA NA UJENZI WA ZAHANATI YA MUUNGANO MUHEZA




Na Oscar Assenga, Muheza

WANANCHI 6,258 wa Kijiji cha Muungano, Wilaya ya Muheza, wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za afya kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ya Muungano, mradi ambao umepokelewa na kuridhiwa na Mwenge wa Uhuru 2026 baada ya kukaguliwa na kupokea taarifa ya utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwang'onda alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Alisema Serikali tayari imepeleka vifaa tiba pamoja na watumishi wa afya watakaotoa huduma katika zahanati hiyo, hatua inayoonesha dhamira ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hususan katika maeneo ya vijijini.

“Mradi huu ni muhimu kwa wananchi wa Muungano na maeneo jirani kwa sababu unasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuongeza ustawi wa jamii,” alisema.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa mafanikio ya mradi huo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hususan Taasisi ya Islamic Help, iliyochangia ujenzi wa zahanati hiyo, huku Serikali ikigharamia vifaa tiba na watumishi wa afya.

Aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kijamii, na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo ili kusaidia kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.

Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akisema kuwa mazingira hayo yanawezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuvutia wadau zaidi kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wake, akitoa taarifa ya mradi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk. Fani Mussa, alisema ujenzi wa Zahanati ya Muungano ulianza Machi 2, 2025 na kukamilika kwa gharama ya Shilingi milioni 165.94.

Alieleza kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 141.55 zilitumika kwa ujenzi, huku Shilingi milioni 24.39 zikitumika kununua vifaa tiba.

Kwa mujibu wa Dk. Mussa, zahanati hiyo itahudumia wakazi 6,258 wa Kijiji cha Muungano, wakiwemo wanaume 3,089 na wanawake 3,169, na inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo.

Baada ya ukaguzi huo, Mwenge wa Uhuru 2026 ulieleza kuridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi huo, ukibainisha kuwa ni hatua muhimu katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya afya nchini.




Post a Comment

0 Comments