Ticker

6/recent/ticker-posts

PPP YATAJWA KUWA NGUZO YA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050

CHUO Kikuu cha Mzumbe kimesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea kwa kiwango kikubwa ushiriki wa sekta binafsi, hususan katika kuzalisha ajira, kuvutia mitaji na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kisasa na wenye ushindani.

Akizungumza leo Juni 26, 2026, wakati wa mhadhara kuhusu "Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP): Nguzo ya Kimkakati katika Kugharamia Mpango wa Nne wa Maendeleo na Dira 2050," Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Mwegoha, alisema sekta binafsi ndiyo itakayokuwa nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ajira nchini.

Amesema tayari chuo kimeanza kuwajengea uwezo watu ndani ya chguo ili nao waweze kuwajengea uwezo Watanzania kuijua na kushiriki katika miradi ya PPP na kuongeza uelewa wa mfumo huo ili wananchi wanufaike na fursa zinazotokana na mwelekeo mpya wa maendeleo.

"Ukisikiliza malengo ya Dira 2050 utaona mchango mkubwa unaotarajiwa kutoka sekta binafsi. Uchumi tunaouelekea unahitaji ushiriki mpana wa sekta hiyo katika uwekezaji, utaalam na uzalishaji wa ajira," amesema.

Profesa Mwegoha amesema Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa kisasa na wenye ushindani, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuchochea maendeleo ya taifa.

Amewataka wanafunzi kusoma kwa kina Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kutumia fursa ya mihadhara hiyo kupata uzoefu kutoka kwa wataalamu wa masuala ya PPP ili wawe sehemu ya viongozi watakaosimamia uchumi wa nchi hapo baadaye.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Hawa Petro, amesema eneo la PPP linafungua fursa mpya kwa wanataaluma na wanafunzi kufanya tafiti zitakazosaidia kutoa suluhisho kwa jamii na kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa miradi ya ubia.

Amesema chuo kimejipanga kushirikiana na wadau wa PPP kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa Watanzania pamoja na kufanya tafiti zitakazosaidia kubaini maeneo yenye fursa na changamoto katika utekelezaji wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Profesa Hawa amesema hatua hiyo itawezesha chuo kutoa mchango mkubwa katika kujenga uelewa wa jamii kuhusu PPP na kuandaa wataalamu watakaosaidia kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments