Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. NDOMBA AWATAKA WATUMISHI DIT KULINDA HADHI YA TAASISI .

 Na Mwandishi Wetu.

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Marco Ndomba, amewataka watumishi wa taasisi hiyo kuanza kutekeleza kikamilifu taratibu za uendeshaji (Standard Operating Procedures - SOPs) na  kuendelea kuzingatia viwango vya ubora katika utekelezaji wa majukumu yao ili kulinda hadhi ya cheti cha ISO 21001:2018 walichokipata mwezi Aprili mwaka huu, ambacho ni ubora wa  kiwango cha kimataifa cha usimamizi wa taasisi za elimu kinacholenga kuhakikisha huduma za ufundishaji, ujifunzaji na uendeshaji wa taasisi zinazingatia ubora unaotambulika duniani.

Akizungumza leo Juni 22, 2026 na watumishi wa DIT katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika kampasi kuu ya Dar es Salaam huku kampasi za Mwanza, Dodoma na Songwe zikifuatilia kwa njia ya mtandao, Prof. Ndomba amesema kuanzia Julai 1 mwaka huu taasisi itaanza kutekeleza kikamilifu taratibu za uendeshaji (Standard Operating Procedures - SOPs) katika maeneo yote ya kazi.

Amesema watumishi wanapaswa kujipanga kwa mabadiliko hayo na kuhakikisha taratibu zinafuatwa kikamilifu katika shughuli za ufundishaji, usimamizi wa mitihani, utawala wa rasilimali watu ikiwemo kupandishwa madaraja watumishi pamoja na huduma nyingine zote za taasisi.

“Sisi tuko ISO Certified sisi wa kimataifa, huduma zetu za kimataifa na tunajali wateja. Cheti cha ISO inasisitiza kujali wateja, na tutakuwa tunakaguliwa kila mwaka na tunaweza tukanyang'anywa, ni jukumu letu sote kama watumishi kuhakikisha tunalinda ubora na viwango" amesema Prof. Ndomba.

Mkuu huyo wa taasisi amewapongeza watumishi wa DIT kwa mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha hivi karibuni, ikiwemo kupata hati safi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu  hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2024/2025, kuendelea kuandaa maandiko bunifu ya miradi na mawazo yaliyowezesha ununuzi wa jengo la NSSF lililogharimu Tsh. Bilioni 21 lenye uwezo wa kuwachukua wanafunzi zaidi ya 3000 , pamoja na maboresho ya miundombinu katika kampasi za  Mwanza na Dodoma.

Aidha, amesema mafanikio hayo yamechangia kuimarika kwa taswira ya DIT nchini, jambo linalodhihirishwa na ongezeko la wanafunzi wanaotaka kujiunga na taasisi hiyo pamoja na pongezi kutoka kwa waajiri wanaoridhishwa na ubora wa wahitimu wake.

Prof. Ndomba amesema moja ya sababu za mafanikio hayo ni utekelezaji wa mfumo wa Teaching Factory ambao unawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo sambamba na mahitaji halisi ya viwanda na sekta ya uzalishaji. Amesema DIT ndiyo taasisi pekee nchini inayotekeleza mfumo huo wa kisasa wa elimu unaopatikana katika taasisi chache za kimataifa.

Amesisitiza kuwa mafanikio yote yaliyopatikana yanapaswa kwenda sambamba na kuimarishwa kwa mifumo ya ubora ili DIT iendelee kuwa kitovu cha umahiri wa teknolojia, ubunifu na mafunzo ya ufundi yanayokidhi viwango vya kimataifa.


























Post a Comment

0 Comments