Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Serikali imeahidi kuendelea kufanya mageuzi ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya utoaji huduma ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, hatua inayolenga kuiwezesha sekta binafsi kuwa injini ya ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Juni 30, 2026 na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alipokuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Mwaka 2026 lililoandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kongamano hilo, Dkt. Nchemba alisema Serikali imejipanga kuhama kutoka mfumo wa kudhibiti biashara kwenda mfumo wa kuwezesha biashara kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji, kupunguza urasimu, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa taasisi zinazotoa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

Alisisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana nayo kwa karibu ili kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanafikiwa.

"Ajenda ya sekta binafsi ni ajenda ya Taifa. Hatuwezi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bila sekta binafsi yenye nguvu, inayowezeshwa na inayoshirikiana kwa karibu na Serikali," alisema.

Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo ya sekta binafsi yanayolenga kuondoa vikwazo vya biashara, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Pia alieleza kuwa amani, utulivu na mshikamano wa Taifa ni msingi muhimu wa ukuaji wa biashara na uchumi, hivyo akatoa wito kwa Watanzania kuendelea kuvilinda ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji na uzalishaji.

Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi, kukuza matumizi ya teknolojia na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa mtazamo wa kuwezesha biashara badala ya kuzikwamisha.

Naye Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Vincent Minja, alisema chemba hiyo imefanya mageuzi ya kiutawala na kidijitali yaliyoboreshwa utoaji wa huduma kwa wanachama, kuimarisha uwakilishi wa sekta binafsi na kuongeza ushindani wa biashara za Tanzania.

Katika kongamano hilo, Waziri Mkuu alizindua rasmi Mfumo wa Kidijitali wa TNCC utakaorahisisha huduma mbalimbali za chemba hiyo, ikiwemo usajili wa wanachama, utoaji wa vyeti vya asili ya bidhaa pamoja na huduma nyingine za biashara kwa njia ya mtandao.

Vilevile, alishuhudia utiaji saini wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano kati ya TNCC na taasisi za umma pamoja na sekta binafsi, hatua inayotarajiwa kuimarisha biashara, uwekezaji, utafiti, ubunifu na maendeleo ya sekta binafsi nchini.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, taasisi za umma, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, mabalozi, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya Tanzania.


Post a Comment

0 Comments