Ticker

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU YAKABIDHI VIFAA TIBA KWA WATOTO WALIOZALIWA KABLA YA WAKATI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA

 


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila (kulia), akimkabidhi Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, vifaa tiba kwa ajili ya watoto njiti vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU.
Na Kadama Malunde – Shinyanga

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekabidhi vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mashine ya kutoa joto kwa watoto wachanga (Radiant Warmer) na mashine ya kutibu ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga (Phototherapy Machine), ambavyo vimenunuliwa kupitia michango ya hiari ya watumishi wa TAKUKURU nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Juni 3, 2026, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, amemkabidhi vifaa hivyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Chalamila amesema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa watumishi wa TAKUKURU katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha huduma za afya nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila.

Amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali na kuboresha miundombinu ya matibabu, jambo ambalo linahitaji kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi.

“Tumeamua kuunga mkono jitihada hizi kwa kununua vifaa tiba kwa ajili ya hospitali mbalimbali nchini. Tayari tumeshatoa vifaa hivi katika mikoa 19, na Shinyanga ni mkoa wa 20. Lengo letu ni kufikia mikoa yote 28 ya Tanzania Bara. Vifaa hivi vimenunuliwa kupitia michango ya hiari ya watumishi wa TAKUKURU,” amesema Chalamila.

Ametoa wito kwa taasisi, mashirika na wananchi wengine kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya, akisisitiza kuwa mahitaji ya vifaa tiba katika hospitali bado ni makubwa.

“Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake. Tunawaomba wadau wengine wajitokeze na kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa michango yao ili kusaidia kuboresha huduma za afya, hususan kwa mama na mtoto,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo akieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza uwezo wa hospitali katika kuwahudumia watoto njiti na wenye uzito mdogo wanaohitaji uangalizi maalum.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akitoa neno la shukrani baada ya kupokea vifaa tiba.

Amesema msaada huo wa TAKUKURU unatarajiwa kuongeza uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga katika kutoa huduma bora kwa watoto wachanga, hususan watoto njiti, na hivyo kuchangia kupunguza vifo vya watoto pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Luzila ameeleza kuwa, Mkoa wa Shinyanga unaendelea kukabiliwa na changamoto ya watoto kuzaliwa kabla ya wakati pamoja na watoto wenye uzito pungufu, hali inayoongeza mahitaji ya vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya huduma za watoto wachanga.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa TAKUKURU na watumishi wake kwa msaada huu mkubwa. Haya ni matendo ya huruma yanayogusa maisha ya watoto wachanga. Vifaa hivi vimekuja katika wakati muafaka na vitasaidia kuboresha huduma tunazotoa kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati,” amesema Dkt. Luzila.

Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za miezi mitatu iliyopita, hospitali hiyo imepokea watoto kadhaa wenye uzito pungufu na waliozaliwa kabla ya wakati, ambapo wengi wao wamefanikiwa kupata matibabu na kurejea katika maisha ya kawaida kutokana na huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Dkt. Luzila pia ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wadau mbalimbali kushiriki katika kuboresha huduma za afya, huku akitoa mwaliko kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia sekta hiyo muhimu.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa tiba kwa ajili ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa tiba vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa tiba vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa tiba kwa ajili ya watoto wachanga vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa tiba kwa ajili ya watoto wachanga vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa tiba kwa ajili ya watoto wachanga vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila (kulia), akimkabidhi Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, vifaa tiba vya kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti), vikiwemo mashine ya joto kwa watoto wachanga (Radiant Warmer) na mashine ya kutibu manjano ya watoto (Phototherapy Machine), vilivyonunuliwa kupitia michango ya hiari ya watumishi wa TAKUKURU.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akitoa neno la shukrani baada ya kupokea vifaa tiba vya kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU.
Muonekano wa baadhi ya vifaa tiba vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na watumishi wa TAKUKURU kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments