Ticker

6/recent/ticker-posts

AJIRA ZA WAZAWA ZILINDWE : CI NYAKUNGA

Na. OWM (KAM), Dar es Salaam

Kamishna wa Uhamiaji wa Divisheni ya Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, CI Fakih Nyakunga, ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) kupitia Idara ya Kazi kuhakikisha vibali vya kazi vinatolewa kwa raia wa kigeni wenye ujuzi ambao haupatikani nchini Tanzania ili kulinda ajira za wazawa.

Nyakunga ametoa kauli hiyo leo Julai 12, 2026, alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026.

Amesema utoaji wa vibali kwa wataalamu wa kigeni wenye ujuzi adimu utatoa fursa kwa Watanzania kujifunza teknolojia na maarifa mapya kupitia ushirikiano kazini, jambo litakalosaidia kuongeza uwezo wa rasilimali watu na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.

Aidha, Kamishna Nyakunga ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa juhudi zake za kutafuta fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi. 

Ameiomba Ofisi hiyo, kupitia Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Sehemu ya Huduma za Ajira, kuendelea kusimamia kwa karibu ustawi wa vijana wanaopata ajira katika mataifa mbalimbali ili kuhakikisha wanapata haki zao na mazingira salama ya kazi.

Kamishna Nyakunga alitembelea na kupata maelezo kuhusu huduma zimazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) yahusuyo mamlaka za mikoa na halmashauri kwenye udhibiti wa maeneo ya mipakani .

Pia alipata maelezo kuhusu elimu ya dawa za kulevya na namna kamisheni ya udhibiti inavyoshirikiana na Idara ya Uhamiaji kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mary Ainiwia kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuwafuatilia Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi kupitia balozi za Tanzania katika nchi husika pamoja na mawakala wa ajira wanaotambulika na Serikali.

Amesema mfumo huo unalenga kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanazingatiwa na kwamba masharti ya mikataba yao ya ajira yanatekelezwa ipasavyo.

Aidha, amebainisha kuwa Sehemu ya Huduma za Ajira hufanya mawasiliano na Watanzania waliopo kazini nje ya nchi kila baada ya miezi mitatu ili kufuatilia maendeleo yao, kupokea changamoto wanazokutana nazo na kuhakikisha waajiri wanazingatia masharti yote ya mikataba ya ajira.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Revocatus Kassimba alimweleza Kamishna Nyakunga kuwa banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu limeendelea kupata mafanikio ya kufikisha elimu na huduma kwa wananchi ambapo mwitikio umekuwa mzuri tangu kuanza kwa maonesho ya 50 ya Sabasaba.

Post a Comment

0 Comments