Ticker

6/recent/ticker-posts

KWAGILWA AFUNGIA KIWANDA CHA HANGJIN STEEL MKURANGA KWA UKIUKWAJI WA SHERIA ZA MAZINGIRA

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, amesimamisha shughuli za Kiwanda cha Hangjin Steel kinachojihusisha na uzalishaji wa nondo kwa kutumia vyuma chakavu, kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, baada ya kubainika kukiuka masharti ya Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Mazingira, ambapo ilibainika kuwa shughuli za kiwanda hicho zilikuwa zinasababisha athari kwa mazingira kutokana na kutokuzingatia masharti yaliyowekwa na mamlaka husika za usimamizi wa mazingira.

Miongoni mwa dosari zilizobainika ni kutokuwepo kwa mfumo wa udhibiti wa taka ndani ya kiwanda, kushindwa kudhibiti mafuta machafu yanayotumika kama chanzo cha nishati na hivyo kuchanganyika na maji na kutiririka kwenye makazi ya wananchi pamoja na mabonde ya maji.

Aidha, kiwanda hicho kilibainika kutokuwa na mfumo madhubuti wa kudhibiti hewa chafu inayozalishwa na shughuli zake, pamoja na kukosa Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) kinachotakiwa kisheria.

Mhe. Kwagilwa ameuagiza uongozi wa kiwanda hicho kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na mamlaka za mazingira kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake.

Maelekezo hayo yanajumuisha kurekebisha dosari zote zilizobainika, kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kutimiza matakwa yote ya kisheria yanayohusu usimamizi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema amepokea maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Naibu Waziri na kuahidi kuwa Baraza hilo litayatekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili kuhakikisha sheria inazingatiwa na mazingira yanaendelea kulindwa.

Post a Comment

0 Comments