Na Issa Mwadangala
Wananchi wa Kata ya Mkwajuni, Wilaya na Mkoa wa Songwe, wameomba Serikali kuongeza na kuboresha alama za usalama barabarani, ikiwemo matuta, ili kupunguza ajali za barabarani katika eneo hilo, ombi hilo limetolewa wakati wa ziara ya Serikali Nyumbani Kwako iliyofanyika katika kata hiyo.
Akizungumza na wananchi Julai 24, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabiri Makame, alisema amepita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na kujionea namna wananchi wanavyothamini kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Vilevile Mh. Makame aliwataka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kusimamia sheria kwa weledi, uadilifu na bila upendeleo, huku wakichukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kukiuka sheria na kanuni za usalama barabarani.
"Kuna mambo matatu ya msingi yatakayosaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo ni kuongeza na kuboresha alama za usalama barabarani, kuendelea kutoa elimu kwa madereva wa bodaboda na watumiaji wengine wa barabara kuhusu matumizi salama ya barabara, pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote wanaokiuka sheria na taratibu za usalama barabarani" alisema Mh. Makame.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, aliwataka wasafirishaji hao kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kuvaa kofia ngumu (helmet) wakati wote, kuepuka kubeba mizigo au abiria kinyume cha sheria, pamoja na kuendesha kwa mwendo unaoruhusiwa, hususan katika maeneo ya makazi, akibainisha kuwa kufanya hivyo kunalinda maisha yao, familia na jamii kwa ujumla.
Akihitimisha, Kamanda Senga aliwataka madereva wote kuachana na tabia ya kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia pombe au vilevi vya aina yoyote, akieleza kuwa vitendo hivyo ni hatari kwa maisha ya dereva na watumiaji wengine wa barabara, huku akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari ili kulinda usalama wake na wa vizazi vijavyo.



0 Comments