Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limeidhinisha kutolewa mara moja kwa takriban dola za Marekani milioni 443.9 kwa Tanzania baada ya kukamilisha tathmini za mwisho chini ya programu za Extended Credit Facility (ECF) inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience and Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika taarifa iliyotolewa Julai 10, IMF imesema uamuzi huo unafuatia kukamilika kwa mapitio ya sita na saba ya mpango wa ECF pamoja na mapitio ya tatu na nne ya mpango wa RSF, ambapo fedha hizo zinajumuisha takriban dola za Marekani milioni 158.75 chini ya ECF na dola za Marekani milioni 298.37 chini ya RSF.
IMF imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara, huku ukuaji wa Pato la Taifa ukifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na kutarajiwa kufika karibu asilimia 6.2 kwa muda wa kati. Sekta zilizotajwa kuchangia matarajio hayo ni pamoja na madini, kilimo na utalii.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, Tanzania imeendelea kudumisha utulivu wa uchumi mpana na mfumuko wa bei umebaki chini, ukiwa asilimia 4.0 mwezi Juni 2026. Hata hivyo, IMF imeonya kuwa kupanda kwa bei za mafuta duniani kunaendelea kutoa shinikizo kwa gharama za maisha na uchumi kwa ujumla.
Taarifa hiyo imeonyesha pia kuwa utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya kiuchumi kwa ujumla ulikuwa wa kuridhisha. Vigezo vingi vya utendaji vilifikiwa kwa wakati, ingawa baadhi ya malengo na mageuzi, hasa katika maeneo ya nishati, usimamizi wa VAT, utawala wa Benki Kuu na uwekezaji wa umma, yalichelewa au hayakukamilika kama ilivyotarajiwa.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Bo Li, alisema Tanzania imefanikiwa kuhifadhi utulivu wa uchumi licha ya misukosuko ya ndani na nje.
Alisema hatua zaidi zinahitajika katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa fedha za umma, na kuongeza uwekezaji katika sekta muhimu kama elimu na afya.
Aidha, IMF imeishauri Tanzania kuendelea na mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha sekta binafsi, na kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Shirika hilo limeonya kuwa kuendelea kwa mzozo wa Mashariki ya Kati kunaweza kudhoofisha ukuaji wa uchumi na kuongeza mfumuko wa bei.
Pamoja na mtazamo chanya wa uchumi, IMF imesisitiza kuwa Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa za kupunguza umaskini, kufikia malengo ya maendeleo endelevu, na kuandaa fursa za kutosha kwa idadi ya watu inayotarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050.
Kwa ujumla, uamuzi wa IMF unaonekana kuwa ishara ya kuendelea kwa imani ya taasisi hiyo kwa mwenendo wa uchumi wa Tanzania, huku ukitoa msukumo mpya kwa Serikali kuharakisha mageuzi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameshukuru uamuzi huo wa Taasisi hiyo kubwa ya Fedha duniani (IMF), kwa kuendelea kuamini mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo nchi imeendelea kupiga hatua kubwa hadi sasa na kuungwa mkono na IMF.
Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu ilipojiunga na IMF tarehe 10 Septemba 1962, ambapo jumla ya ahadi ya mikopo na misaada ya IMF kwa Tanzania imefikia Dola ya Marekani bilioni 4.578. Kati ya kiasi hicho, portfolio hai ya sasa ni dola za Marekani bilioni 2.52.

0 Comments