Ticker

6/recent/ticker-posts

WAHITIMU 191 WATUNIKIWA VYETI KOLANDOTO, BODI YASUKUMA HADHI YA CHUO KIKUU


Sehemu ya wahitimu 191 wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto katika Mahafali ya 69 ya chuo hicho.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Dkt. Joseph Mayala, akizungumza wakati wa Mahafali ya 69 ya chuo hicho.
Sehemu ya wahitimu 191 wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto katika Mahafali ya 69 ya chuo hicho.
Sehemu ya wahitimu 191 wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto katika Mahafali ya 69 ya chuo hicho.
Sehemu ya wahitimu 191 wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto katika Mahafali ya 69 ya chuo hicho.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Paschal Shiluka, akizungumza wakati wa Mahafali ya 69 ya chuo hicho.
Katibu Mkuu wa AICT, Josephales Mtembe, akizungumza wakati wa Mahafali ya 69 ya Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto.


Jumla ya wahitimu 191 wametunukiwa vyeti katika ngazi za Astashahada na Shahada katika Mahafali ya 69 ya Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, huku Bodi ya Wakurugenzi ya chuo hicho ikiitaka menejimenti kuharakisha mchakato wa kukipandisha hadhi kuwa chuo kikuu ili kuongeza uwezo wa udahili na kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya afya nchini.

Mahafali hayo yamefanyika huku chuo hicho kikieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi, programu za mafunzo pamoja na mchango wake katika kuzalisha wataalamu wanaohitajika katika sekta ya afya.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo Julai 24,2026, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Dkt. Joseph Mayala, amesema hatua ya kukipandisha hadhi chuo hicho kuwa chuo kikuu ni muhimu katika kuongeza fursa za elimu ya juu ya afya na kukidhi mahitaji ya wataalamu katika soko la ajira.

Dkt. Mayala amesema kupandishwa hadhi kwa chuo kutakiwezesha kuongeza programu za masomo, kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuimarisha mchango wake katika kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya afya.

“Tunataka kuona mchakato wa kukipandisha hadhi chuo hiki unakamilika kwa wakati ili kiweze kuongeza uwezo wake wa kutoa elimu ya juu na kuzalisha wataalamu wengi zaidi watakaohudumia jamii,” amesema Dkt. Mayala.

Aidha, amesema Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo la Kolandoto ikiwemo ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka barabara kuu hadi chuoni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema miradi hiyo itakapokamilika itasaidia kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma, kurahisisha usafiri kwa wanafunzi, watumishi na wagonjwa wanaofika katika Hospitali ya Kolandoto, sambamba na kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa AICT, Josephales Mtembe, amesema Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kimeendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Kanisa la AICT ya kuleta maendeleo kwa jamii kupitia sekta za elimu, afya na huduma za kijamii.

Amesema tangu kuanzishwa kwake, chuo kimepiga hatua kubwa ikiwemo kuongeza programu za masomo kutoka programu moja hadi saba, jambo linaloonyesha ukuaji wa taasisi hiyo na mchango wake katika kuandaa wataalamu wa afya.

Naye Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Paschal Shiluka, amesema chuo hicho kimeendelea kukua kwa kasi ambapo idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 12 wakati wa kuanzishwa hadi kufikia wanafunzi 3,350 kwa sasa.

Amesema ongezeko hilo linaonesha imani ya jamii katika ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho pamoja na mchango wake katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza idadi ya wataalamu wa afya nchini.

Shiluka amesema pamoja na mafanikio hayo, chuo bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo hitaji la kukamilishwa kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo pamoja na uboreshaji wa barabara inayounganisha chuo na hospitali kwa kiwango cha lami.

Ameongeza kuwa chuo hicho kitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kinaimarika zaidi na kuwa taasisi yenye uwezo mkubwa wa kutoa elimu ya afya yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya ndani na kimataifa.

Wakati huo huo, wahitimu waliotunukiwa vyeti wamehimizwa kwenda kuitumikia jamii kwa weledi, uadilifu na kuzingatia maadili ya taaluma zao, huku wakikumbushwa kuepuka vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa sheria ambavyo vinaweza kuathiri heshima ya taaluma walizosomea.

Mahafali hayo yamehitimisha safari ya kitaaluma kwa wahitimu hao huku yakitoa taswira ya mchango unaoendelea kutolewa na Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto katika kuimarisha rasilimali watu kwenye sekta ya afya nchini.




Post a Comment

0 Comments