Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU NA MWENYEKITI AL MANSOUR HOLDING WATETA MASUALA YA UWEKEZAJI, AJIRA NA MAENDELEO YA UJUZI

Na: OWM (KAM) – Doha, Qatar

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Al Mansour Holding, Mhe. Sheikh Mansour, leo tarehe 10, 2026 jijini Doha, Qatar ambapo wamejadili kuhusu ushirikiano katika maeneo ya uwekezaji, ajira na maendeleo ya ujuzi.

Aidha, katika mazungumzo yao Mhe. Sangu alitumia fursa hiyo kumueleza Mwenyekiti wa Al Mansour Holding dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuendelea kuweka mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji pamoja na kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Qatar.

Vilevile, Waziri Sangu ameipongeza kampuni ya Al Mansour Holding kwa kuendelea kuongeza wigo wa uwekezaji katika Mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania Bara na Zanzibar. Pia, amehamasisha kampuni hiyo kutumia wataalamu na nguvu kazi ya Watanzania katika shughuli zake nchini Qatar na katika masoko mengine ya kimataifa.

Kadhalika, ameihakikishia kampuni hiyo ushirikiano katika kukuza maendeleo ya rasilimali watu kupitia mafunzo, uhamishaji wa teknolojia na ujuzi ili kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi.

Katika ziara hiyo, Waziri Sangu ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Awesi Mohamed, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Khalid Masoud Waziri, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Rashid Ali Salim, pamoja na wataalamu wengine kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments