NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Atupele Mwambene ametoa wito kwa walimu walioshiriki mafunzo ya somo la Elimu ya Biashara kuonesha ushirikiano kwa walimu wataowakuta katika vituo vyao vya kazi ili kuwasaidia watoto katika malezi pamoja na ujifunzaji.
Ametoa wito huo leo Agosti 21, 2026 wakati akihitimisha mafunzo ya somo la Elimu ya Biashara kwa walimu wa kujitolea waliofadhliwa na Shirika lisilo la kiserikali la EDUCATE, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Nkurumah chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Bw. Mwambene amesema, ili kufikia malengo ya kuboresha elimu katika mazingira mtayoenda msisite kuomba ushauri na miongozo ya kiutendaji kwa viongozi na wenyeji mtaowakuta jambo litaloimarisha upendo na ushirikiano katika kutimiza wajibu wa malezi na ufundishaji kwa wanafunzi.
"Kubwa ninalotaka kusema katika eneo hili ni mkawaheshimu , mkaishi kwa nidhamu , mkaishi kwa ushirikiano na pale ambapo mtakua mmekwama kwasababu ya mazingira mtayoenda ni mapya, msisite kuwaomba miongozo na ushauri ili nyote kwa pamoja mkaweze kutekeleza jukumu la malezi ya watoto wetu kwa ufanisi, " amesema Bw. Mwambene.
Ameendelea kusisitiza kuwa, nafasi za ajira zilizotolewa, ni sehemu ya mkakati wa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu nchini kuboresha ujifunzaji na ufundishaji kwa watoto, hivyo kuwataka walimu hao kwenda kutekeleza kile ambacho wawezeshaji kutoka TET na EDUCATE wamewafundisha kwa siku kumi na mbili (12) ili kikalete matokeo chanya katika Sekta ya Elimu.
Aidha, Bw. Mwambene amewataka washiriki wa mafunzo hayo kwenda kuwajibika vyema kwa viongozi wao katika maeneo waliyopangiwa na kufuata taratibu za kiutumishi katika kutatua changamoto zao ili kupata suluhishi bora kwa pande zote.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema, katika kutekeleza mtaala ulioboreshwa Serikali ilisuka upya somo la commerce ili kumfundisha mwanafunzi mbinu ma mikakati ya kutumia ujuzi alioupata katika masomo mengine kuweza kuanzisha na kuendesha Biashara kwa ufanisi
Ameendelea kusema, baada ya kusuka somo hili sasa linaitwa somo la Elimu ya Biashara, na kusisitiza kuwa, somo hili ni moja ya masomo ya lazima kwa wanafunzi wote wa ngazi ya Sekondari ya chini katika mkondo wa Amali na Jumla.
Nae mwakilishi kutoka Shirika lilolakiserikali la EDUCATE Bw. Neilson amesema, katika mafunzo ya siku 12 walimu wameandaliwa vyema katika kutekeleza ufundishaji wa somo la Elimu ya Biashara kwa kuzingatia Mtaala unaozingatia umahiri ambapo utekelezaji utasaidia wanafunzi kutambua changamoto na kuzigeuza kuwa fursa za ujasilia mali ambao utachangia kukuza uchumi wa nchi.






















0 Comments