Ticker

6/recent/ticker-posts

TIMU YA STANBIC YASHIRIKI MASHINDANO YA BASKETBALL YA WACHINA KUDHIBITISHA USHIRIKIANO

 

Na Mwandishi Wetu 

Dar es Salaam, Tanzania – Jumamosi, 1 Agosti 2026: Katika hatua ya kipekee ya kuonyesha ushirikiano wa dhati, Stanbic Bank Tanzania sio tu imedhamini Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina kwa Shilingi milioni 30, bali pia imetoa timu yake kushiriki moja kwa moja mashindanoni.

Mashindano hayo yamefunguliwa rasmi katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga, na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, ambaye alishuhudia ukabidhi wa hundi ya udhamini.

Ushiriki wa timu ya Stanbic umeonekana kama ishara ya uhusiano imara uliopo kati ya benki hiyo na jamii ya Wachina nchini, huku michezo ikitumika kama daraja la kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kijamii na kubadilishana tamaduni.

Mashindano hayo yamekuwa jukwaa la kuleta pamoja wafanyabiashara wa Kichina, viongozi wa jamii na wadau mbalimbali katika mazingira ya urafiki na ushirikiano.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Corporate and Investment Banking) wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema uamuzi wa kushiriki kama mdhamini na pia mshindani unaonyesha dhamira ya benki ya kuwa karibu na jamii.

"Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa muhimu kwetu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee. Dhamira hiyo ndiyo msingi wa kazi yetu kupitia Standard Bank Group, ushirikiano wetu na ICBC pamoja na dawati letu maalum la huduma kwa wafanyabiashara wa Kichina," alisema Manase.

Aliongeza kuwa:"Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Tunaendelea kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja, na tunajivunia kushirikiana tena na jamii ya Wachina mwaka huu."

Kwa upande wake, Bw. Gerson Msigwa alipongeza Stanbic Bank kwa kuendelea kuunga mkono mashindano hayo na kusema michezo imekuwa chombo muhimu cha kuimarisha urafiki kati ya Tanzania na China.

"Uhusiano kati ya China na Tanzania una historia ndefu na unaendelea kuimarika kupitia matukio kama haya ambapo michezo inatuunganisha katika roho ya urafiki na kuheshimiana. Ushirikiano wa namna hii kati ya sekta binafsi na jamii unachangia kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa mataifa yetu mawili," alisema.

Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Wachina yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya biashara, kuimarisha mahusiano na kukuza kubadilishana uzoefu wa kitamaduni kati ya wadau kutoka Tanzania na China.

Kadri ushirikiano huo unavyoendelea kukua, Stanbic Bank itaendelea kuimarisha uhusiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania pamoja na kuunga mkono majukwaa yanayochochea ushirikiano, maelewano na maendeleo ya pamoja.





Post a Comment

0 Comments