Ticker

6/recent/ticker-posts

WATUHUMIWA 153, WAHAMIAJI HARAMU 47 WAKAMATWA SHINYANGA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi.

***
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekamata jumla ya watuhumiwa 153 wanaodaiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya uhalifu, huku wahamiaji haramu 47 nao wakikamatwa katika misako na operesheni zilizofanyika mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema operesheni hizo zililenga kuimarisha usalama, kudhibiti vitendo vya uhalifu pamoja na kuwakamata watu wanaojihusisha na shughuli zinazokiuka sheria.

Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, katika operesheni hizo Jeshi la Polisi lilikamata vielelezo mbalimbali, ikiwemo noti bandia zenye thamani ya Shilingi milioni 1.53, mirungi kilogramu 43, bangi kilogramu 380, pikipiki 26, mifuko 13 ya saruji, nondo 20, mbao 70, baiskeli moja na mtungi mmoja wa kuzimia moto.

Aidha, Jeshi la Polisi limekamata wahamiaji haramu 47 waliodaiwa kuingia nchini bila kuwa na vibali halali. Watuhumiwa hao wamefikishwa katika hatua za kisheria kwa mujibu wa makosa wanayodaiwa kutenda.

Katika upande wa usalama barabarani, Kamanda Magomi amesema jumla ya makosa 5,291 yamebainika katika operesheni za Kikosi cha Usalama Barabarani.

Kati ya makosa hayo, 4,079 yalihusu magari, huku 1,212 yakihusisha bajaji na pikipiki.

Pia, madereva sita wamechukuliwa hatua baada ya kubainika kuendesha magari kwa mwendokasi wa hadi kilomita 116 kwa saa. Leseni zao zimefungiwa kama hatua ya kuwaonya madereva wengine wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Kamanda Magomi amesema hatua mbalimbali za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wahusika, zikiwemo faini za papo kwa papo, huku makosa makubwa yakipelekwa katika hatua nyingine za kisheria.

Mbali na misako na operesheni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na uhalifu.

Elimu hiyo imejikita katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, kuimarisha ulinzi shirikishi, kuzingatia maadili kwa vijana, pamoja na kuwahimiza madereva kutii sheria za usalama barabarani.

Jeshi hilo pia limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na watu wanaohatarisha usalama wa jamii.

Kamanda Magomi amesisitiza kuwa usalama wa jamii unahitaji ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Aidha, Jeshi la Polisi limewakumbusha madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani wakati wote ili kupunguza ajali na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.

Post a Comment

0 Comments