Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, amekutana na Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Barnabas Michael Taligunga kwa ajili ya kujadili changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji zinazowakabili wananchi katika Kata ya Mailimoja, ,Pangani, Msangani na Viziwaziwa zilizopo ndani ya Manispaa ya Kibaha.
Akizungumza katika kikao hicho,Mstahiki Meya Manispaa ya Kibaha Dkt. Nicas amewataka wananchi wa kata zenye changamoto ya maji kuwa na uvumilivu wakati mamlaka husika ikiendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto hizo.
Dkt Nicas Mawazo amesema,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan tayari ametoa fedha kwenye miradi ya maji na tayari Dawasa wapo kazini na Kata hizo zitaanza kupata maji ikiwemo Kata ya Pangani ambapo mradi wa ujenzi wa tenki unatarajia kumalizika mwezi wa Februari, 2027 .
Aidha, Dkt Nicas amewapongeza DAWASA kwa juhudi inazofanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji, huku akisisitiza kuwa uongozi wa Manispaa utaendelea kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi na kushirikiana na mamlaka husika.
Meneja wa DAWASA, Mhandisi Barnabas Taligunga amewasilisha maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kata mbalimbali zikiwemo Kata Viziwaziwa , Pangani , Mailimoja na Msangani zinazowakabili wananchi akisisitiza umuhimu wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika katika maeneo hayo.
Aidha, mhandisi Barnabas amesema katika Kata ya Pangani wanatarajia mradi wa ujenzi wa tanki la maji kuisha mwezi wa 2, 2027 hivyo ni muhimu kuhakikisha eneo ilo wananchi wanapata maji kwa haraka kwa kufunga booster ili kusukuma maji kwenda kwa wananchi kabla ya kumalizika kwa mradi huo.
Akizungumzia kuhusu mkakati wa haraka wa kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji, amesema wanatarajia kufanya ujenzi wa boosterstation ambao una uwezo wa kusambaza maji kwa haraka katika maeneo yenye changamoto wakati wakiendelea na mchakato wa msukumo wa maji na mabomba.
Mhandisi Barnabas,amesema mamlaka hiyo imepokea changamoto hizo na ipo tayari kuendelea kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na uongozi wa Manispaa ya Kibaha na itaendelea kuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya maji na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aidha, ameeleza kuwa DAWASA itaendelea kufuatilia maeneo yenye changamoto na kuhakikisha hatua zinazohitajika zinachukuliwa ili kukamilisha changamoto zinazowakabili wananchi wa Manispaa ya Kibaha.




0 Comments