Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuimarisha utunzaji wa mazingira kuelekea mvua za El Niño, likisema utupaji holela wa taka na uharibifu wa miundombinu ya maji unaweza kuongeza hatari ya mafuriko.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa NEMC, Martha Kawishe, amesema mvua ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa, lakini baadhi ya shughuli za kibinadamu zinaweza kuongeza athari za mvua kubwa endapo hazitasimamiwa ipasavyo.
Amesema utupaji wa taka kwenye mifereji, mito na makorongo, pamoja na kuziba kwa njia za maji, ujenzi katika njia za asili za maji na uharibifu wa maeneo oevu ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza hatari ya mafuriko.
Kawashe amesisitiza kuwa maeneo ya mabondeni, kingo za mito, maeneo yenye miteremko mikali na maeneo yenye mifumo duni ya kupitisha maji yanahitaji uangalizi na tahadhari zaidi.
Kwa mujibu wa NEMC, wananchi wanapaswa kuhakikisha taka haziingii kwenye mifereji na njia nyingine za maji, huku Mamlaka za Serikali za Mitaa zikihakikisha mifereji na njia za kupitisha maji zinasafishwa na kubaki wazi.
Aidha, Baraza limesisitiza umuhimu wa kulinda kingo za mito, mabonde na maeneo oevu, pamoja na kuchukua hatua za kuzuia mmomonyoko wa udongo unaoweza kuchochewa na mvua kubwa.
NEMC pia imewataka waendelezaji wa miradi, viwanda, vituo vya mafuta, migodi, hospitali na maeneo yanayohifadhi kemikali au taka hatarishi kuhakikisha vifaa na taka hizo zinasimamiwa kwa usalama ili kuzuia kusombwa na maji ya mafuriko na kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji na makazi ya wananchi.
Baraza limesema litaendelea kushirikiana na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine kutoa elimu, kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mazingira, pamoja na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya shughuli zinazoharibu mazingira.
NEMC imewahimiza wananchi kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kuchukua hatua mapema, ikisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni sehemu muhimu ya kupunguza athari za mvua kubwa na mafuriko.
0 Comments