Dar es Salaam, Septemba 3, 2026
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mhandisi Bruno Tarimo, amewahimiza mama na baba lishe kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida na kuhamia katika nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao, kuhifadhi mazingira na kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Mhandisi Tarimo ametoa wito huo leo, Septemba 3, 2026, wakati wa mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia yaliyotolewa na PBPA kwa mama na baba lishe wa Kikundi cha Jitihada, yaliyofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, PBPA imewakabidhi mama na baba lishe 70 jumla ya tani 1.7 za mkaa mbadala.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa PBPA, Mhandisi Tarimo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya ushiriki wa Wakala katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10, uliozinduliwa mwaka 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wamehama kutoka katika matumizi ya nishati zisizo safi na salama na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
“Tumekuja kushirikiana na mama na baba lishe pamoja na watoa huduma wa teknolojia za nishati safi ili kuwapatia elimu kuhusu matumizi yake na kuwasaidia kuachana na nishati zisizo safi na salama,” amesema Mhandisi Tarimo.
Ameeleza kuwa PBPA imeanza na mama na baba lishe wa Kurasini kwa sababu eneo hilo lina makampuni mengi ya mafuta ambayo ni miongoni mwa wadau wakuu wa Wakala. Wafanyakazi wa makampuni hayo hupata huduma za chakula kutoka kwa mama na baba lishe wanaofanya biashara katika maeneo ya Kurasini na Kigamboni.
“Wafanyakazi wanapokuja kula wataona chakula kimepikwa katika mazingira safi, hakina moshi na kina ladha nzuri. Wanaweza pia kuifikisha elimu hii kwa ndugu, jamaa na marafiki. Kwa namna hiyo, tunaendelea kuchangia utekelezaji wa lengo la kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania,” amesema.
Mhandisi Tarimo amesema, katika mafunzo hayo, washiriki walipata fursa ya kuona na kujifunza matumizi ya majiko ya kisasa ya umeme, majiko banifu na mkaa mbadala. Pia walishuhudia kwa vitendo namna teknolojia hizo zinavyoweza kutumika kupika chakula kwa haraka, bila kutoa moshi mwingi wala kuchafua vyombo vya kupikia.
Amesema matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida yana madhara kwa afya za watumiaji, hususan mama na baba lishe ambao hukaa karibu na moshi kwa muda mrefu. Aidha, matumizi ya nishati hizo yanachangia uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti.
PBPA pia inaendelea kuzihamasisha taasisi zinazohudumia au kuandaa chakula kwa zaidi ya watu 100 kwa siku kuhamia katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Jitihada, Bw. Lugano Mwaiswelo, amesema mafunzo hayo yamewapatia washiriki maarifa yatakayowasaidia kulinda afya zao na kuboresha mazingira wanamofanyia biashara.
“Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuwakumbuka mama na baba lishe kupitia jitihada za kuhamia katika nishati safi ya kupikia inasaidia kuboresha mazingira na kulinda afya zetu. Tumepokea elimu hii kwa furaha, tutazingatia tuliyofundishwa na tutakuwa mfano kwa vikundi vingine kwa kutumia majiko banifu, mkaa mbadala na majiko ya umeme,” amesema Bw. Mwaiswelo.
Mmoja wa mama lishe walioshiriki mafunzo hayo, Bi. Joyce Benjamin Mtweve, amesema maonesho ya upishi yaliyofanyika yamewathibitishia kuwa matumizi ya nishati safi yanaweza kurahisisha kazi zao na kuboresha mazingira ya biashara.
“Tumefurahi sana kwa ujio wenu na kwa kutuonesha majiko ya nishati safi. Tumeshuhudia yakipika vizuri, bila moshi na bila kuchafua sufuria. Tuko tayari kuunga mkono juhudi hizi,” amesema Bi. Mtweve.
Naye Rais wa Mama Lishe Tanzania, Bi. Latifa Habibu Masasi, amesema upatikanaji wa gesi, majiko ya umeme, majiko banifu na mkaa mbadala umewapa mama lishe fursa ya kuchagua teknolojia inayolingana na mahitaji pamoja na uwezo wao.
“Nishati safi ni muhimu sana. Teknolojia hizi zinaongeza thamani katika mnyororo wa biashara ya chakula kwa sababu zinawawezesha mama lishe kupika kwa haraka, kwa wakati na katika mazingira salama zaidi,” amesema Bi. Masasi.
Mafunzo hayo yanaashiria kuanza kwa kampeni ya PBPA ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia miongoni mwa mama na baba lishe nchini. Kampeni hiyo inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine yenye mama na baba lishe wanaotoa huduma za chakula kwa wadau wa PBPA.








0 Comments