Na MWANDISHINWETU, Iringa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kuwa mfano wa demokrasia nchini, kikisisitiza kuwa misingi hiyo inaanza ndani ya Chama chenyewe.
CCM imesema imekuwa ikizingatia misingi ya demokrasia katika uendeshaji wa shughuli zake, ikiwemo katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara, Stephen Wasira alipokuwa akifungua mafunzo ya Iitikadi na uenezi kwa makada wa Chama yaliyofanyika katika Chuo cha CCM, mkoani Iringa, jana.
Wasira akisema uchaguzi unaofanyika ndani ya CCM unalenga kutoa nafasi kwa wanachama kushiriki katika kuwachagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuhakikisha misingi ya demokrasia inaendelea kuimarika ndani ya Chama.
Aidha, alivitaka vyama vingine vya siasa nchini kuiga mfano huo kwa kuhakikisha vinazingatia demokrasia katika shughuli zake na uchaguzi wa viongozi wao.
Makamu Mwenyekiti Wasira alisisitiza kuwa, demokrasia ni muhimu katika kujenga vyama imara, vinavyoweza kuwajibika kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, alisema CCM haiwezi kuingilia mihimili ya dola kwa kuwa kila mhimili una majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na sheria.
Alieleza kuwa, Mahakama ni miongoni mwa mihimili inayopaswa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na kwa kuzingatia sheria.
Wasira alibainisha kwamba, kuheshimu mgawanyo wa madaraka ni sehemu muhimu ya uendeshaji wa nchi kwa misingi ya kikatiba.
Hivyo siyo sahihi kwa chama cha siasa kuingilia utekelezaji wa majukumu ya Mahakama au mhimili mwingine unaotambulika kikatiba.
Pia, alisisitiza umuhimu wa kila taasisi kufanya kazi kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa na Katiba na sheria za nchi.
Misingi hiyo inalenga kulinda utawala wa sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Alisisitiza CCM kuendelea kusimamia demokrasia ndani ya Chama na kuheshimu taasisi nyingine za kikatiba katika utekelezaji wa majukumu yake.
Sambamba na hayo, aliwataka wadau wa siasa kuendelea kujenga mazingira ya kuheshimiana na kufuata sheria katika shughuli zao.
Kwa ujumla, CCM imesema dhamira yake ni kuendelea kuwa mfano wa demokrasia ndani ya Chama, huku ikiheshimu mgawanyo wa madaraka na uhuru wa mihimili mingine ya dola.



0 Comments