Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema matumizi sahihi ya Akili Unde (AI) yanaweza kuboresha elimu na tafiti kwa kuwasaidia wanafunzi na watafiti kubaini mapengo ya tafiti (research gaps), kupata mwelekeo wa utafiti na kuongeza ubora wa kazi zao, akisisitiza kuwa teknolojia hiyo inapaswa kutumiwa kwa kuzingatia uadilifu na maadili ya kitaaluma.
Akizungumza katika kongamano la kitaaluma lililofanyika IAA, Kampasi ya Dar es Salaam, na kurushwa kwa njia ya mtandao katika kampasi nyingine, Prof. Sedoyeka amesema AI ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utafiti, ikiwa itatumika kwa lengo la kuongeza maarifa na ujuzi badala ya kuchukua nafasi ya uwezo wa mwanafunzi kufikiri na kufanya kazi mwenyewe.
Prof. Sedoyeka amesema hayo huku akieleza kuwa makongamano ya kitaaluma yanayoandaliwa na IAA, yanatoa fursa kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili kuwasilisha, kujadili, kutetea na kuchapisha matokeo ya tafiti zao, akiweka wazi kuwa kongamano hilo la siku mbili limewakutanisha wanafunzi na wataalamu kutoka fani mbalimbali ili kuwapa washiriki nafasi ya kuwasilisha kazi zao, kupata maoni ya kitaalamu na mwongozo wa kuboresha tafiti kabla ya kuzichapisha.
“Mwanafunzi anapokamilisha utafiti anatakiwa kuandika andiko la kitaaluma (research paper). Ili kuhitimu, anatakiwa pia kuhakikisha andiko lake linachapishwa. Sasa ili kuwapa wanafunzi wote fursa ya kuwasilisha, kutetea na kuchapisha tafiti zao, tunaandaa makongamano haya ya kitaaluma,” amesema Prof. Sedoyeka.
Hata hivyo, Prof. Sedoyeka amesisitiza kuhusu matumizi ya AI, akisema teknolojia hiyo haipaswi kuonekana kama tatizo iwapo inamsaidia mwanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaohitajika kufikia malengo ya kitaaluma, huku akihimiza matumizi yake kwa kuzingatia sheria na maadili ya kitaaluma.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Shahada ya Uzamili walioshiriki kuwasilisha tafiti zao katika kongamano hilo, akiwemo Shalfan Zuberi na Imtithal Salum Tawfiq, wamesema wanazingatia uhalisi na ubora wa tafiti zao kabla ya kuziandaa kwa ajili ya kuchapishwa, wakieleza kuwa tafiti walizowasilisha zinalenga kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, hususan katika sekta za mawasiliano, uchukuzi na miundombinu.










0 Comments