Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeeleza kuwa lina nafasi muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa sera ya viwanda kupitia uandaaji wa viwango, utoaji wa elimu kwa wazalishaji pamoja na kusogeza huduma za upimaji na uthibitishaji wa bidhaa karibu na wananchi.
Shirika hilo limesisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya viwanda hayawezi kutenganishwa na masuala ya viwango, kwa kuwa bidhaa zinazozalishwa zinapaswa kukidhi matakwa ya ubora ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Akizungumza kuhusu mchango wa TBS katika utekelezaji wa sera ya viwanda, Meneja wa Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka, amesema shirika hilo linaendelea kuwahamasisha wazalishaji kushiriki katika mchakato wa uandaaji wa viwango ili kuhakikisha vinavyoandaliwa vinaendana na mahitaji ya uzalishaji pamoja na teknolojia inayotumika viwandani.
Amesema pia wazalishaji ambao tayari wamepata uthibitisho wa ubora wa bidhaa zao wanapaswa kuendelea kuzingatia viwango vilivyowekwa ili kudumisha ubora na ushindani wa bidhaa zao sokoni.
Kaseka amesema TBS inaendelea kutoa huduma na elimu kwa wajasiriamali wadogo ili kuwajengea uwezo wa kukua na kuwa wamiliki wa viwanda vikubwa siku zijazo.
Amesisitiza kuwa hakuna tofauti katika matakwa ya viwango kati ya mjasiriamali mdogo na mkubwa, kwani kila bidhaa inayozalishwa inapaswa kukidhi matakwa ya ubora ili kulinda afya na usalama wa watumiaji.
Ameongeza kuwa bidhaa zinazokidhi viwango zina fursa kubwa ya kuingia katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa, hivyo ni muhimu kwa wajasiriamali wadogo kuzingatia ubora tangu hatua za awali za uzalishaji.
Katika hatua nyingine, amesema TBS imeweka mikakati ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga maabara katika kila kanda ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za upimaji na uthibitishaji wa bidhaa kwa wazalishaji wa mikoa inayozunguka maeneo hayo.
Vilevile, shirika hilo linaendelea kuandaa viwango vipya kwa kuzingatia mahitaji ya soko, maoni ya wadau wa viwanda pamoja na mabadiliko ya teknolojia ili kuhakikisha viwango vinavyoandaliwa vinaendana na mazingira ya sasa ya uzalishaji.
TBS imeendelea kuwakumbusha wafanyabiashara na wajasiriamali kutembelea banda lake lililopo katika Viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma kwa ajili ya kupata elimu kuhusu viwango, huku wajasiriamali wadogo wakihimizwa kutumia dawati maalumu lililotengwa kwa ajili ya kuwahudumia.



0 Comments