Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe imefungua sehemu ya barabara ya Forodha (OSBP) Tunduma yenye urefu wa mita 400, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliyetoa wakati wa ziara yake mkoani humo, akitaka kasi ya ujenzi wa mradi huo iongezwe.
Mradi huo wa upanuzi na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege una urefu wa jumla ya mita 1,675. Sehemu iliyofunguliwa ina upana wa mita 14, kuanzia mpaka wa Tanzania na Zambia hadi mzunguko wa Tunduma (Roundabout), huku ujenzi wa sehemu iliyobaki yenye urefu wa mita 1,275 ukiendelea kuelekea Mbeya. Sehemu hiyo itakuwa na upana wa mita saba na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Novemba 2026.
Akizungumza na wananchi wakati wa ufunguzi wa barabara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Aboubakar Kunenga, ameitaka TANROADS kuendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Amesisitiza kuwa miradi ya maendeleo inapaswa kutekelezwa kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Silvan Mloka, amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 6.8 umefikia hatua za mwisho za utekelezaji, ambapo njia mbili kati ya nne zimefunguliwa kwa matumizi ya wananchi, huku njia mbili zilizobaki zikitarajiwa kufunguliwa ndani ya wiki mbili zijazo.
Amesema mradi huo unalenga kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia, kwa kuboresha mtiririko wa magari, kuongeza ufanisi wa huduma za forodha na kuchochea biashara ya kikanda.
Wananchi na watumiaji wa barabara hiyo, akiwemo Elisha Isambo, Dominic Kaimba na Pauli Ng'umbi, wameishukuru Serikali kwa hatua ya kufungua sehemu ya barabara hiyo, wakieleza kuwa itapunguza muda wa safari, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo, kukuza biashara, kuongeza fursa za ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo la Tunduma na maeneo jirani.
Wamesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara, madereva wa malori na wananchi wanaotumia mpaka wa Tunduma kufanya shughuli zao za kila siku.










0 Comments