Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

TANZANIA YATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA VYUO VYA UFUNDI NA VIWANDA


Tanzania imetakiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi stadi na sekta ya viwanda ili kuwawezesha wahitimu kupata ajira, kujiajiri na kutumia ipasavyo ujuzi wanaoupata wakati wa mafunzo.

Wito huo umetolewa na wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi wakati wa Mkutano wa Usambazaji wa Matokeo na Hitimisho la Mradi wa TVET@Work, uliojadili mafanikio ya mradi huo pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vya ufundi na waajiri.

Wadau hao wamesema pamoja na ongezeko la fursa za mafunzo ya ufundi, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha wahitimu wanapata mazingira yatakayowawezesha kutumia ujuzi walioupata katika maeneo ya kazi na hatimaye kupata ajira.

Meneja wa Mradi kutoka Chuo Kikuu cha HAMK cha Finland, Carita Cruz, amesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele ni utekelezaji wa miongozo iliyotengenezwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na waajiri.

Amesema miongozo hiyo inalenga kuweka mfumo madhubuti utakaowezesha vyuo na viwanda kushirikiana katika kutoa mafunzo ya vitendo yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Ameeleza kuwa kuingizwa kwa mpango huo katika Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni hatua muhimu inayoonesha umuhimu wake katika kuimarisha mfumo wa elimu ya ufundi nchini.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa miongozo hiyo ni muhimu zaidi kuliko kuwepo kwake kwenye nyaraka, kwani utasaidia kubaini mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji maboresho.

Cruz amebainisha kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi wanaosimamia uratibu wa ushirikiano kati ya vyuo na viwanda, akisema jukumu hilo halipaswi kuachiwa mtu mmoja pekee, bali linahitaji kushirikisha wataalamu mbalimbali ndani ya taasisi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa waajiri kufahamu mitaala inayotumiwa na vyuo vya ufundi ili kuhakikisha mafunzo wanayowapatia wanafunzi katika maeneo ya kazi yanaendana na ujuzi wanaofundishwa darasani.

Kwa upande wake, Irene Kanyankole kutoka HakiElimu, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, amesema mradi wa TVET@Work umechangia kuimarisha uwezo wa wakufunzi, matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, elimu ya ujasiriamali, mafunzo kwa vitendo viwandani na ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta ya viwanda.

Amesema maeneo hayo ni muhimu katika kuwaandaa vijana kukabiliana na ushindani wa soko la ajira, kwa kuwa wahitimu wanahitaji zaidi ya ujuzi wa kitaalamu, ikiwemo ubunifu, uwezo wa kutatua changamoto, ujuzi wa kidijitali na maadili ya kazi.

Kanyankole amesisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya shughuli zilizotekelezwa pekee, bali kwa kuangalia mabadiliko yaliyopatikana na namna taasisi zitakavyoendeleza mbinu na mifumo iliyoanzishwa baada ya mradi kumalizika.

Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni kuimarisha uwezo wa taasisi kuratibu ushirikiano na viwanda, kuwaandaa wakufunzi wa maeneo ya kazi kuwalea na kuwaelekeza wanafunzi, pamoja na kuhakikisha mitaala inazingatia mabadiliko ya mahitaji ya uchumi.

Naye Dkt. Zuhura Juma Ali kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume (KIST), Zanzibar, amesema ushirikiano wa karibu kati ya vyuo vya ufundi na viwanda ni msingi wa kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Amesema mafunzo ya ufundi hayapaswi kuishia darasani, bali wanafunzi wanapaswa kupata fursa za kujifunza katika mazingira halisi ya kazi ili kujenga uzoefu, kufahamu matumizi ya teknolojia za kisasa na kuzielewa changamoto za maeneo ya kazi.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo pia utaziwezesha taasisi za mafunzo kubaini mapungufu ya ujuzi unaohitajika na waajiri na kufanya maboresho ya mitaala ili kuendana na mahitaji ya sekta husika.

Mradi wa TVET@Work ulizinduliwa Januari 25, 2024, kwa ushirikiano wa HakiElimu, Chuo Kikuu cha HAMK cha Finland, 3DBear, VETA, KIST na Centro San Viator (CSV), kwa ufadhili wa pamoja wa Umoja wa Ulaya.

Mradi huo ulilenga kuongeza uwezo wa vijana kuajirika na kujiajiri kupitia uimarishaji wa uwezo wa wakufunzi, matumizi ya teknolojia za kidijitali katika ufundishaji, elimu ya ujasiriamali na kujenga uhusiano imara kati ya taasisi za mafunzo na sekta ya ajira.

Post a Comment

0 Comments