Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMBA AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI SAUDI ARABIA


Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa pili kulia) akiwa katika mazungumzo na Mhadisi Adil Saleh Alomair, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati Jadidifu (wa kwanza kushoto) na Mhandisi Faisal Ali Al Swayed kutoka kampuni ya Advanced Electronics Company (wa pili kushoto) katika Makazi ya Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia. Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Ally J. Mwadini.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo na Mhandisi Faisal Ali Al Swayed kutoka kampuni ya Advanced Electronics Company (kushoto) huku Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio (wa kwanza kulia), Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja (wa pili kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia Balozi Ally J. Mwadini wakifuatilia kwa makini mazungumzo hayo.

***************************

Riyadh, Saudi Arabia,Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amewasili nchini Saudi Arabia kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mualiko wa Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhe Abdulaziz bin Salman Al Saud.Akiwa nchini humo Waziri Makamba anatarajiwa kushiriki hafla ya uzinduzi wa “Saudi Green Initiative” utakaofanyika Riyadh tarehe 23 Oktoba 2021 pamoja na kufanya mikutano ya kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya Nishati nchini Tanzania.Mapema baada ya kuwasilia nchini humo, Waziri Makamba alikutana na kufanya mazungumzo na Mhandisi Faisal Ali Al Swayed kutoka kampuni ya Advanced Electronics Company na Mhandisi Adil Saleh Alomair, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati Jadidifu (Renewable Energy).Akizungumza na Mha. Faisal Ali Al Swayed, Waziri Makamba alisema “Tanzania imepiga hatua kubwa katika usambazaji wa nishati za gesi asilia na umeme lakini bado kuna uhitaji wa vifaa kama vile mita za kisasa za Gesi Asilia na Umeme kuendana na kasi ya usambazaji na teknolojia kwa ujumla”.Aidha, Waziri Makamba alieleza nia ya Serikali kutumia zaidi teknolojia kukomesha tatizo la wizi na upotevu wa nishati jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuwapatia wananchi nishati ya uhakika.“Moja ya kazi kubwa tuliyonayo sasa ni kuangalia namna tunaweza kutumia teknolojia kukomesha changamoto hii” alieleza Waziri Makamba na kuwakaribisha wataalamu hao kutembelea Tanzania kwa lengo la kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya Nishati.Kwa upande wake Mha. Faisal alimhakikishia Waziri Makamba kuwa kampuni yake ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mita kwa kuzingatia mahitaji ya mteja na kuahidi kuendelea kuwasiliana na Ubalozi kwa lengo la kuwekeza nchini Tanzania.Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati, January Makamba ameambatana na Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio.

Post a Comment

0 Comments