Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI HAITAVUMILIA VITENDO VYA UKATILI WOWOTE WA KIJINSIA – MAJALIWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha Mwongozo wa Kushughulikia Ukatili wa Kijinsia katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati baada ya kuuzindua kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Novemba 25, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamisi na kulia ni Wakili Anna Meeda Kulaya ambaye ni Mratibu wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua Mwongozo wa Kushughulikia Ukatili wa Kijinsia katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati nchini , kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Novemba 25, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamisi na kulia ni Wakili Anna Meeda Kulaya ambaye ni Mratibu wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia kwenye ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, Novemba 25, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamisi (kulia) wakati alipoingia kwenye ukumbi wa Mlimani City Dar es salaam kuzindua Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza katika uzinduzi huo kwenye ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, Novemba 25, 2021. (Picha na ofisi ya Waziri mkuu)

*****************************

Ø Aagiza kuanzishwa madawati ya kijinsia katika shule za msingi na SekondariWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsi na haitavumilia aina yoyote ya ukatili wa kijinsia utakaofanywa na mtu yeyote hapa nchini.Mheshimiwa Majaliwa amesema, Mheshimiwa, Rais Samia Suluhu Hassan tayari amejipambanua na ameweka bayana msimamo wake dhidi ya ukatili wa kijinsia na kusisitiza umuhimu wa kubadili fikra na kufanya harakati zote kwa ushirika kati ya wanaume na wanawake ili kujenga jamii yenye amani upendo na usawa.“Lazima jamii yetu ijenge msukumo wa kuhakikisha kuwa kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani ukatili wa kingono kama vile rushwa ya ngono, ukatili baina ya wenza, ubakaji, mimba na ndoa za utotoni”.Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 25, 2021) katika Uzinduzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.Amesema vitendo vya ukatili vinatokea katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika ngazi ya Kaya, mahali pa kazi, maeneo ya biashara kama masoko lakini pia shuleni na mahali pengine katika jamii zetu.“Sote tunafahamu kwamba, licha ya sheria kali zilizopo bado vitendo vya ukatili vinaendelea kuwa ni changamoto kubwa na hivyo nguvu ya pamoja inahitajika katika kukemea vitendo hivyo”.Mheshimiwa Majaliwa ametanabaisha kuwa Serikali itaendelea kutilia na kuunga mkono hatua zote stahiki katika kutokomeza ukatili wa kijinsia katika ngazi zote na itaongeza kasi ya kuhamasisha jamii kubadili fikra na mitazamo hasi inayochochea vitendo vya ukatili.“Nitoe wito kwenu wananchi na wadau wa masuala ya jinsia kushirikiana na Serikali katika kuwekeza katika afua za kutokomeza ukatili wa kijinsia”.Akizungumzia kampeni hiyo ya siku 16 za harakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia amesema Tanzania kwa kushirikiana na mataifa mengine itaendelea kuadhimisha kampeni hiyo ili kutokomeza kabisa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.“Ninafahamu kuwa, huu ni mwaka wa 24 wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia hapa nchini. Nitumie fursa hii kuwahakishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuungana na mataifa mengine kupambana na ukatili wa kijinsia”.Amesema katika kufanikisha Usawa wa Kijinsia kwa jamii ya watanzania Serikali imeendelea kuimarisha u jenzi wa vituo vya kijamii vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Kuanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi ambapo hadi sasa yapo madawati 420, Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Mkakakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji nchini.Waziri Mkuu alihitimisha kwa kuagiza, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuandaa mpango mpya; Kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za ukatili katika ngazi zote; Kusimamia utekelezaji wa sera na sheria hususan Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, pamoja na kusimamia uendeshaji wa usimamizi wa Mahakama ya Familia ili kuimarisha ushughulikiaji wa migogoro ya ndoa na familia.Naye, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, amesema Wizara itaendelea kusimamia miongozo yote inayotolewa na wadau pamoja na washirika wa masuala ya jinsia ili kuhakikisha inapunguza kama sio kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia.Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Kitengo cha Wanawake, Hodan Addou amesema dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kijinsia hususani katika kipindi cha ugonjwa wa Uviko 19 kwani watu wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi mitandaoni na wahanga wakubwa wa udhalilishaji wa mitandaoni wamekuwa wanawake na watoto.Awali, Mratibu wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF) Anna Kulaya, amesema Mtandao huo unaunga mkono na kupongeza hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kuruhusu watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua pamoja na kuanzishwa kwa mahakama maalum ya masuala ya familia ili kukuongeza upatikanaji wa haki kwa wanawake.

Post a Comment

0 Comments