Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAJIVUNIA MCHANGO WA OFISI YA MSAJILI HAZINA UKUAJI KIUCHUMI

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro (katikati) akijumuika na watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo, jana jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), tawi la Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri. Wengine kutoka kushoto ni Pili Mazowea, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Ofisi ya Msajili wa Hazina na Waziry Mkumbo, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.( _Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)
Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza jambo wakati wa mkutano wa kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa Mwaka 2021/22 jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro (katikati) aliyefungua mkutano huo na kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), tawi la Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri. ( Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro, akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina uliofanyika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam, jana ( _Picha na Ofisi ya Msajili wa Hazina)


******************************


Na Mwandishi Wetu


SERIKALI imesema itaendelea kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina bila kuchoka, kwa kuwa ofisi hiyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.


Aidha, imeipongeza ofisi hiyo kwa kazi nzuri ya usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma, maeneo ambayo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa ili hatimaye uweze kuleta tija na kuendelea kutoa mchango wa ukuaji kiuchumi na kustawisha maendeleo ya nchi.


Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa Mwaka 2021/2022, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza baada ya kukaribishwa na Mwenyekiti wa Mkutano huo, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto, Dk Ndumbaro alisema; “Ni ukweli usiopingika kuwa kutokana na majukumu makubwa ya kusimamia takribani Mashirika na Taasisi za Umma 237, Kampuni 50 ambako Serikali imewekeza mtaji wake kwa utaratibu wa Hisa pamoja na kusimamia jumla ya Mashirika ya Umma, Viwanda na Mashamba 341 yaliyobinafsishwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.”


Aliongeza kuwa, watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wanapaswa kuzingatia kuwa nchi inawategemea katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kupunguza matumizi na kuimarisha Utawala Bora kupitia usimamizi madhubuti wa Mashirika na Taasisi za Umma, hivyo ili kufikia malengo hayo, wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu.


“Kila mtumishi katika Ofisi ya Msajili wa Hazina anapaswa kutambua wajibu wake kwa Taifa na kujitambua kuwa ana umuhimu katika kuwezesha Taifa kufikia malengo yake.


“Endeleeni kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, weledi na uzalendo mkubwa katika kusimamia rasilimali za umma mlizopewa dhamana ya kuzitunza na kusimamia ili zilete tija na kuongeza mapato yasiyo ya kodi kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali kuwa na uwezo wa kuboresha huduma kwa wananchi na maslahi ya Watumishi wote,” alisema.


Awali, akimkaribisha Dk Ndumbaro, Msajili wa Hazina alimshukuru yeye binafsi kwa kukubali mwaliko na kushiriki kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, lakini pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini ofisi yake katika usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma.


Kipekee, Mgonya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Msajili wa Hazina ili kuendeleza jukumu la usimamizi wa rasilimali za nchi zinazotokana na Uwekezaji wa Serikali.


“Ahadi yangu kwa Mheshimiwa Rais Samia ni kwamba; kwa kushirikiana na watumishi wenzangu na tukimshirikisha Mungu, tutatekeleza kwa ukamilifu jukumu tulilopewa kwa uaminifu mkubwa. Tumejipanga vyema kuhakikisha kazi ya usimamizi wa Mashirika ya Umma inaleta tija na kwamba kwa dhamana hii tuliyokabidhwa tutaisimamia kikamilifu na kwa weledi,” alisema Mgonya.


Katika mkutano huo, Msajili wa Hazina aliwasilisha mambo mbalimbali ambayo ofisi imeyatekeleza katika kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma, lakini pia aliwasilisha mikakati iliyopo katika kuimarisha usimamizi kwenye Mashirika na Taasisi za Umma ili mchango wa uwekezaji wa Serikali uweze kuleta tija kwa maendeleo ya nchi.


Alisema ufanisi wa usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina umejidhihirisha katika maeneo mengi, akitolea mfano ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kuwa, katika kipindi cha miaka minne cha kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21 mapato yameongezeka kutoka Sh. Bilioni 161.03 mwaka 2016/17 hadi Sh. Bilioni 637.67 mwaka 2020/21.


Kwa mujibu wa Mgonya, mapato haya ni yale tu yanayopitia akaunti za Ofisi ya Msajili wa Hazina na kwamba endapo yangejumuisha na yale yanayokwenda moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, yangepaa zaidi akitolea mfano kabla ya janga la UVIKO-19, mapato yalifikia Sh Trilioni 1.052 mwaka 2018/19.


Alisema utekelezaji wa masuala mbalimbali na mikakati iliyopo inakwenda sambamba na kaulimbiu ya mkutano huo; “Usimamizi Bora wa Mashirika ya Umma unachangia Kuimarisha Uchumi wa Nchi; Maslahi ya Watumishi yaboreshwe.”

Post a Comment

0 Comments