Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. NDALICHAKO AKAGUA MRADI WA VIJANA, KITALU NYUMBA MANISPAA YA SINGIDA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako (wa pili kulia) akipata maelezo leo Septemba 17, 2022 kutoka kwa Kiongozi wa Wanufaika wa mradi wa Kitalu Nyumba, Emmaculatha Nkumbi (katikati) wakati wa ziara yake ya siku moja ya kukagua mradi huo wa kilimo cha mbogamboga na matunda wenye thamani ya Sh. 30 Milioni unaotekelezwa Manispaa ya Singida.Kutoka kushoto ni mnufaika wa mradi huo, David Nyitika, Madania Juma na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Ally Mwendo.
Wanufaika wa mradi huo Madania Juma na David Nyitika (kulia) wakiwajibika katika Kitalu Nyumba.
Muonekano wa Kitalu Nyumba hicho kilichopo Manispaa ya Singida.
Muonekano wa Kitalu Nyumba hicho kwa nje.
Miche ya matunda ikiandaliwa nje ya Kitalu Nyumba hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako (wa pili kushoto) akipata maelezo wakati wa ziara hiyo.
....................................................


Dotto Mwaibale na Philemon Mazala , Singida


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amekagua mradi wa Kitalu Nyumba wa kilimo cha mbogamboga na matunda wenye thamani ya Sh. 30 Milioni unaotekelezwa Manispaa ya Singiga.

Akikagua mradi huo leo Septemba 17, 2022 alisema ameridhishwa na utekelezaji wake na kueleza kwamba Manispaa ya Singida ni miongoni mwa wilaya zilizofanya vizuri kati ya wilaya 117.

Ndalichako alisema mradi huo unafadhiliwa na ofisi ya Waziri Mkuu kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alielekeza kubuniwa kwa miradi itakayoweza kuwakomboa vijana kiuchumi na kuwapa ujuzi.

"Miradi ya namna hii inatekelezwa katika mikoa 17 ambapo pia tumezifikia halmashauri za wilaya 117 na vijana takribani 12,000 wamenufaika na mafunzo ya mradi huu wa kitalu nyumba na fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya mafunzo hayo ni Sh. 5.3 Bilioni" alisema Ndalichako.

Ndalichako alisema vijana wamekuwa wakifurahia mradi huo na kuwa wataendelea kumpigia hodi Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kusaidia mradi huo wa kuwawezesha vijana.

Aidha Ndalichako alisema programu ya kuwajengea ujuzi vijana kwa mwaka 2022/ 2023 Serikali imetenga Sh. 9 Bilioni na katika mafunzo wanayotegemea kuyafanya ni maeneo maalumu ambayo wanafuga samaki kama kule Ziwa Victoria.

Alisema katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kujenga vituo Atamizi vitano ambavyo vitakuwa na vifaa vya usindikaji na uchakataji wa mazao mbalimbali na kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana wanapewa fursa ya kuomba mkopo ili kuongeza thamani ya mazao hayo na Serikali itapitia maombi hayo kuona kama yatakidhi vigezo.

Ndalichako alisema kumekuwa na tabia ya vijana kushindwa kurejesha mikopo ya asilimia 10 wanayopewa na halmashauri hivyo kutokana na hali hiyo hivi sasa wamependekeza wawe wanakopeshwa vifaa kulingana na mahitaji yao na baadaye kurejesha mkopo huo.

"Nina waagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi kuhakikisha wanatoa mikopo hiyo kwa vijana kwani ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kila robo ya mwaka mnatakiwa kufanya hivyo" alisema Ndalichako.

Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2022/ 2023 kupitia mfuko wa Waziri Mkuu zimetengwa Sh.Bilioni 1 kwa ajili ya kuwakopesha vijana hivyo wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo.

Akizungumzia kuhusu mkopo wa asilimia 10 alisema zamani ulikuwa ukitolewa kwa vikundi lakini hivi sasa wameweka uratibu wa kumpa mtu yeyote ambaye atakuwa na sifa kulingana na jambo analotaka kulifanya baada ya kulifanyia ubunifu.

Mratibu wa mradi huo Manispaa ya Singida, Simon Magige alisema walipokea vifaa vya ujenzi wa kitalu nyumba na fedha za kuendesha mafunzo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 30 Milioni.

Alisema jumla ya vijana 100 wamenufaika na mradi huo 20 kati yao wakipata mafunzo ya utengenezaji wa kitalu nyumba huko 80 wakiwa wamepata mafunzo ya uzalishaji wa mbogamboga kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba kibiashara (Kilimo Biashara).

Post a Comment

0 Comments